







Na Mwamvua Mwinyi, Mkuranga
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amezindua mradi wa basi dogo la kikundi cha vijana wanane cha UNAMA, kinachojishughulisha na usafirishaji wa abiria ,kijiji cha Picha ya Ndege, kata ya Vikindu wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Mradi huo wenye thamani ya sh. milioni 85.2 umetokana na fedha za asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri, ukiwa na lengo la kuwaunganisha vijana wanaojishughulisha na usafirishaji ili kujiongezea kipato.
Akizindua mradi huo Aprili 24, 2026, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Mkuranga, Mwang’onda amewahimiza vijana nchini kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega, amesema kuwa upatikanaji wa mikopo kwa vijana unawawezesha kujiajiri kupitia miradi ya kiuchumi.
“Tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza utoaji wa fedha katika halmashauri, pamoja na kusisitiza ukusanyaji wa mapato ya ndani unaowezesha kutengwa kwa asilimia 10 kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,” amebainisha Ulega.
Vilevile, Ulega ameeleza wataendelea kutenga fedha kupitia vikao vya halmashauri ili kuwezesha makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasir, akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, amesema jumla ya miradi nane yenye thamani ya sh. milioni 39.5 imepitiwa mwaka 2026.
Ameelezea miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa usambazaji wa nishati safi ya kupikia, kiwanda cha vinywaji baridi cha Yaket International, ujenzi wa uzio wa Shule ya Sekondari Mwinyi, ujenzi wa boksi kalavati, sanjali na mradi wa maji katika kijiji cha Sotele.
Leo ni siku ya saba tangu Mwenge wa Uhuru upokelewe mkoani Pwani Aprili 18, 2026, ambapo unatarajiwa kuendelea na mbio zake Aprili 25, 2026 katika Wilaya ya Kibiti.


