RAIS wa Marekani Donald Trump amesema kuwa vizuizi dhidi ya Iran vinaweza kudumu kwa miezi kadhaa, hatua iliyosababisha bei za mafuta kupanda kwa kiwango cha juu hapo jana katika kipindi cha miaka minne.

Katika mkutano wake na wakuu wa sekta ya mafuta, Trump alidai kuwa mzingiro wa bandari za Iran una ufanisi mkubwa kuliko mashambulizi ya mabomu. Tehran imesisitiza kuwa Marekani ni lazima ikomeshe mzingiro huo kabla ya kufikia makubaliano yoyote.

Trump alisema kwamba anakataa pendekezo la Iran la kufungua upya Mlango bahari wa Hormuz kwa sharti la kuondolewa vizuizi vya Marekani, mpango ambao ungeahirisha majadiliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.


Aidha pia waziri wake wa Ulinzi Pete Hegseth, alikabiliana na wabunge wa Democrats kuhusu vita vya Iran siku ya Jumatano, katika ushahidi wake wa kwanza mbele ya Bunge tangu Rais Donald Trump alipoanzisha mgogoro huo miezi miwili iliyopita.

Akihojiwa mbele ya Kamati ya bunge inayohusika na masuala ya Kijeshi, Hegseth aliulizwa maswali kadhaa ikiwemo gharama za vita hivyo na ikiwa alizingatia hatari ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz endapo ingeshambuliwa na alijibu kwamba, “Pentagon ilitathmini vipengele vyote vya hatari hiyo”.

Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ilishindwa kuzuia kufungwa kwa mlango huo, jambo lililosababisha kupanda kwa bei ya mafuta na madhara ya kiuchumi kote duniani. Kuhusu gharama za vita waziri huyo alisema hadi kufikia sasa inakadiriwa kuwa chini ya dola bilioni 25.