Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Dar es Salaam

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amezitaka Wakala wa Barabara Mijini na Vijini TARURA,Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhusisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika hatua za ujenzi wa majengo, ili kuhakikisha kunakuwa na nafasi za kutosha kwa ajili ya kupita magari ya zimamoto wakati wa dharura.

Msando alitoa kauli hiyo Mei 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Zimamoto Duniani, yanayoadhimishwa kila mwaka kwa kaulimbiu isemayo, “Chukua tahadhari leo kuokoa maisha na mali kwa ajili ya kesho.”

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Jeshi la Zimamoto na taasisi hizo utasaidia kuboresha mipango ya ujenzi na kupunguza hatari ya majanga, hususan ajali za moto ambazo mara nyingi husababishwa na ujenzi holela usiozingatia kanuni na taratibu.
Aidha, Msando alikemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kufanya miunganisho holela ya umeme, akieleza kuwa hali hiyo ni hatari kubwa kwa usalama wa maisha na mali.

“ Kumekuwa na uunganishaji wa umeme holela, hasa katika maeneo ya biashara. Unakuta nyaya zimepitishwa katika maeneo hatarishi na mita zinaunganishwa bila kuzingatia usalama. Ni lazima ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema Msando.

Pia amegusia changamoto ya ucheleweshaji wa huduma za zimamoto wakati wa majanga, akibainisha kuwa mara nyingi hali hiyo husababishwa na ukosefu wa miundombinu rafiki, ikiwemo barabara nyembamba au kukosekana kabisa, kutokana na ujenzi usiopangwa.

Amefafanua kuwa licha ya magari ya zimamoto kuwa tayari kufika katika maeneo ya tukio, hushindwa kupenya kutokana na majengo kujengwa kwa kubanana bila kuacha njia za kupita.

Kwa upande wake, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, SACF Mabusi Peter, amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani yalitokana na tukio la mwaka 1999 nchini Australia, katika eneo la Linton, Jimbo la Victoria, ambapo wazimamoto watano walipoteza maisha wakijaribu kuzima moto mkubwa wa msitu.

Alifafanua kuwa tukio hilo liliibua hisia za kimataifa na kusababisha kuanzishwa kwa siku maalum ya kuwaenzi mashujaa wa zimamoto waliopoteza maisha wakitekeleza majukumu yao, ambapo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 4.

Aidha, alisema maadhimisho hayo yanatambua mchango mkubwa wa askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kulinda maisha na mali za wananchi dhidi ya majanga mbalimbali yakiwemo moto, mafuriko, matetemeko ya ardhi, maporomoko ya ardhi pamoja na ajali za barabarani.

Aliongeza kuwa nchini Tanzania, jeshi hilo limeendelea kuonesha weledi, ushujaa na uzalendo katika kukabiliana na majanga makubwa, ikiwemo tukio la watu kuzama katika Ziwa Rukwa Januari 2025, maporomoko ya matope Hanang mkoani Manyara Desemba 2023, mafuriko ya Rufiji mkoani Pwani Aprili 2014, kuporomoka kwa jengo Kariakoo jijini Dar es Salaam, pamoja na moto wa misitu katika Mlima Kilimanjaro na Sao Hill mkoani Njombe katika nyakati tofauti.

Maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukumbusha jamii umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga, pamoja na kuthamini mchango wa wazimamoto katika kuokoa maisha na mali za wananchi.