Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. John Jingu, amepokelewa rasmi na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Juma Homera kufuatia uhamisho uliofanywa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Akizungumza baada ya mapokezi hayo yaliyofanyika Mtumba Jijini Dodoma Mei 06,2026, Waziri Homera amempongeza Dkt. Jingu kwa kuendelea kuaminiwa na kumkaribisha rasmi huku akieleza kuwa Wizara ina majukumu muhimu yenye mchango mpana katika maendeleo ya Taifa ikiwemo usimamizi wa utawala wa sheria na utoaji wa huduma za kisheria kwa Umma.
Aidha Dkt Homera amebainisha kuwa Uongozi, Menejimenti na watumishi wapo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
“Niwaombe kila mmoja wenu atoe ushirikiano kwa Katibu Mkuu katika kufanya kazi. Tuongeze bidii na mshikamano ili kufanikisha majukumu ya wizara hususan katika kutoa huduma kwa Watanzania katika sekta ya Sheria. “Amesema Waziri Homera.
Kwa upande wake, Dkt. Jingu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa dhamana ya kuhudumu katika nafasi hiyo, na ameeleza kuwa ataendelea kufanya kwa kujituma na kuzingatia misingi ya uwajibikaji ili kufikia malengo ya wizara kwa kushirikiana na Viongozi, Menejimenti na Watumishi.








