Na Theophilida Felician, JamhiriMedia, Kagera

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji EWURA CCC Mkoa Kagera limefanikiwa kuwafikia wananchi 1143 katika suala zima la kuwapatia elimu ya huduma hizo.

Ameitoa kauli hiyo afisa mwandamizi wa baraza hilo mkoa Kagera Anadorice Komba wakati akizungumza na chombo hiki ofisi za EWURA CCC zilizopo manispaa ya Bukoba.

Afisa huyo awali amezitaja njia zilizotumika kuwafikia wananchi ni pamoja na kushirikishwa kwenye mikutano ya mitaa inayoandaliwa na viongozi wa mitaa, watendaji, shule za sekondari, vituo vya waendesha pikipiki, vyombo vya habari na baadhi ya taasisi za umma ambapo jumla ya maeneo 49 yamefikiwa na baraza hilo kwa mwaka huu wa bajeti unaoisha muda wake.

Hata hivyo amefafanua kuwa katika kipindi hicho wamepokea malalamiko 247 maji yakiwa 161, umeme 85 na mafuta 1 ambapo kwa kiwango kikubwa malalamiko hayo waliyafikisha kwa watoa huduma na baadhi kufikishwa kwa mdhibiti hivyo malalamiko hayo yalitatuliwa na wananchi wanaendelea kupata huduma ipasavyo.

Amesema baraza hilo hufuatiria kwa ukaribu taarifa zinazotolewa na wananchi ili kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati na watoa huduma ambapo amewashukuru watoa huduma wa mamlaka husika kwa namna wanavyotoa ushirikiano wakutosha katika kufanyia kazi taarifa za wananchi pindi zinapotolewa na baraza hilo na wananchi kwa ujumla huku akiwasihi kutoa huduma bora kwa wananchi jambo ambalo litasaidia kuyaondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Ametoa wito kwa wananchi kuitumia EWURA CCC kupata elimu na mambo mengine ikiwemo ya utoajia taarifa wanapokuwa na changamoto za huduma.

Amehitimisha akisisitiza kuwa Baraza hilo lenye kauli mbiu isemayo huduma bora ni haki yangu,haki yangu ni huduma bora linaendelea na juhudi mbalimbali ili kuwafikia wananchi kwa lengo la kuwaelimisha zaidi.