Na Theophilida Felician, JamhuriMedia

Taasisi ya International Peace information (IPI) imewateua mabalozi wa amani watakaofanya kazi yakuitangaza amani nchini na nje ya nchi.

Akizungumza hayo na Jamhuri Digital juzi makao makuu ya IPI yaliyopo mkoani Dar es salaam Rais wa taasisi hiyo Prof. Wilson George Munguza amesema kuwa taasisi hiyo ambayo imejikita zaidi kuhamasisha amani nchini imeendelea kutumia njia mbalimbali kuitangaza amani lengo ikiwa nikuunga mkono juhudi za serikali ili kuhakikisha amani ya nchi inakuwa tulivu na kudumu nyakati zote.

Rais Munguza amefafanua kuwa mabalozi hao miatano walioteuliwa kwa awamu ya kwanza wanaendelea kunolewa kwa muda wa miezi miwili ili kuongezewa mbinu na maarifa zaidi kwa lengo la kuwaweka sawa na kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa.

Aidha amesema taasisi imelenga kuwapeleka mabalozi katika nchi za Afrika mashariki hususani zenye kukabiliwa na migogoro ya ukosefu wa amani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwingineko.

Hata hivyo ameongeza kuwa licha ya kuwateuwa mabalozi tayari taasisi imewateua wabunge wa amani ambao wanaendelea kusaidiana majukumu na wabunge wa majimbo ambapo hivi karibuni taasisi imemtunuku tuzo ya pongezi spika wa bunge Mussa Azzan Zungu ikiwa nisehemu ya kutambua juhudi zake katika kuzisimamia vyema shughuli za bunge hilo tukufu.

Amehitimisha akiishukuru serikali inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ambapo amewaomba viongozi wa wilaya, mikoa na wengine kuwapatia ushirikiano mabalozi wa amani watakapokuwa wameanza majukumu maeneo watakayopangiwa kote nchini.