Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

KAMATI ya Siasa Mkoa wa Pwani imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Chalinze, ikieleza kuwa miradi hiyo imekuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kuongeza vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo.

Kamati hiyo imepongeza hatua ya halmashauri kuendelea kuwekeza katika vitega uchumi mbalimbali, huku ikieleza kuwa ipo katika mipango ya kujenga mradi wa Machinga Complex pamoja na kituo kikubwa cha mafuta ili kuongeza vyanzo vipya vya mapato .

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa hospital ya wilaya ya Msoga na vyumba 82 vya biashara stendi ya mabasi Chalinze, Mwenyekiti wa Kamati ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Pwani Mwinshehe Mlao, alisema Halmashauri ya Chalinze ni mfano wa kuigwa kutokana na namna inavyotenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi .

Aidha, Mlao alisema kamati hiyo imeridhishwa na upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Msoga ambao umepokea bilioni moja katika mwaka wa fedha 2025/2026.

“Naijua hospitali hii tangu ikiwa zahanati mwaka 1983 hadi sasa imepandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Msoga, tumeridhishwa na ubora wa ujenzi na weledi wa wataalamu wake”

” Tunampongeza Mkuu wa Mkoa, viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo na watendaji wote waliosimamia mradi huu,” alieleza Mlao.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Kamisaa , Abubakar Kunenge, alisema Mkoa wa Pwani una nafasi kubwa ya kimkakati kiuchumi na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya na kutenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Msoga, Dk. Isdory Mfugale, alifafanua hospitali hiyo ni miongoni mwa vituo 64 vya kutolea huduma za afya Chalinze.

Alibainisha hadi sasa ujenzi wa hospitali hiyo umetumia zaidi ya sh milioni 911, huku majengo mengi yakiwa yamekamilika isipokuwa jengo la wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) utekelezaji umefikia asilimia 85 .

Vilevile Kamati hiyo ilikagua na kuridhishwa na mradi wa ujenzi wa vyumba 82 vya biashara, kantini, baa, uzio pamoja na jengo la mama lishe katika stendi ya mabasi Chalinze.

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Ismail Bilali, alisema mradi huo ulitarajiwa kugharimu milioni 640.5 ambapo hadi sasa zaidi ya milioni 604.5 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri zimetumika kutekeleza mradi huo.