Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, George Masaju amewataka vijana nchini kutumia vipaji, ubunifu na maarifa waliyopewa ili kuchangia maendeleo ya taifa badala ya kusubiri kuajiriwa pekee.


Jaji Masaju amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha ‘Sing Gratitude’ kilichoandikwa na Wakili Msomi, Bi. Aisha Saidi Kingu, ambapo alisema vijana ndiyo nguvu kazi muhimu inayotegemewa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia nchini.
Alisema kupitia sanaa, sayansi na bunifu mbalimbali, vijana wana nafasi kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa na kusaidia taifa kujikomboa kutoka kwenye utegemezi wa mataifa yaliyoendelea.

“Katika dunia ya sasa teknolojia imekua kwa kasi kubwa, hivyo vijana mnayo nafasi pana ya kutumia vipaji na ubunifu mlionao ili taifa liweze kunufaika na mchango wenu,” Alisema Jaji Masaju.

Aidha, alimpongeza Bi. Aisha kwa kutumia kipaji chake cha uandishi kwa kuelimisha jamii kupitia mashairi yaliyomo kwenye kitabu hicho, akisema ni mfano bora wa kuigwa kwa vijana wengine nchini.

Kwa mujibu wa Jaji huyo Mkuu, matumizi sahihi ya vipaji yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na vizazi vijavyo.

Sambamba na hilo, aliwataka vijana kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu ili kuongeza maarifa, uwezo wa kufikiri na kujiamini katika maisha yao ya kila siku.

“Kusoma vitabu kunapanua fikra, kunaongeza weledi na humjenga mtu kuwa na mchango wenye matokeo chanya kwa taifa. Vijana wajifunze kupitia mifano kama ya Bi. Aisha,” Alisisitiza Jaji Masaju.

Pia aliwahimiza wananchi na vijana kwa ujumla kukisoma kitabu hicho akieleza kuwa kina ujumbe mkubwa wa maisha unaohamasisha umuhimu wa kushukuru kwa kila hatua ya maisha.

Awali, mwandishi wa kitabu hicho, Bi. Aisha , alisema ‘Sing Gratitude’ ni zawadi kwa Watanzania wote kwa kuwa mashairi yake yanagusa makundi mbalimbali ya jamii bila ubaguzi.

Alisema jamii inapaswa kujifunza umuhimu wa kuwa na moyo wa shukrani kwani kufanya hivyo kunajenga matumaini, imani na mtazamo chanya wa maisha.

“Ninaamini kitabu hiki kitasaidia kubadilisha fikra za watu wengi na kuwafanya waone umuhimu wa kushukuru kwa kila jambo katika maisha yao,” Alisema Bi. Aisha.

Aidha, aliwataka vijana kuondokana na uvivu wa kusoma vitabu akisema elimu inayopatikana kupitia usomaji ni silaha muhimu ya kujikomboa dhidi ya fikra hasi na kukata tamaa.

Naye Mhadhiri Msaidizi wa Sheria za Biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Wakili Msomi Yusto Habiye, ambaye ndiye mhariri wa kitabu hicho, alisema kazi hiyo imebeba mafunzo yenye tija kwa jamii kuhusu umuhimu wa shukrani na uvumilivu katika maisha.

Alisema mwandishi ameonyesha uwezo mkubwa wa kutumia sanaa ya uandishi kuhamasisha jamii kujitambua na kuthamini vipaji walivyopewa.

“Kitabu hiki ni chachu ya mabadiliko kwa vijana na jamii kwa ujumla. Kinatoa ujumbe wa matumaini, uthubutu na umuhimu wa kutumia vipawa kwa maendeleo ya taifa,” Alisema Wakili Habiye.
Kwa upande wake Baba mzazi wa Bi. Aisha Dkt. Saidi Kingu amesema anajivunia kipaji cha binti yake kwani jitihada zake na juhudi anazozifanya sasa zilianza kuonekana tangu kipindi cha utoto wake ambapo kipaji chake kiligundulika akiwa darasa la nne alipoanza kutumia madaftari ya shule kwaajili ya kuandika mashairi yake kisha mwalimu wake Bi. Yasinta Mwambashi kukiona kipaji hicho na kutoa taarifa kwa wazazi wake.
Anasema Aisha aliendelea na utunzi wa mashairi hayo hata baada ya kuanza elimu ya sekondari na baadaye elimu ya juu ambako ndiko aliko jipambanua na kuonesha uwezo wake kwa kuanza kuyaboresha mashairi yake aliyoyaandika kabla na hatimaye kuanza kuandika maishairi ya viongozi na watu mashuhuri.
“kwa kipindi hicho ilitushangaza sana kwani alikua bado mdogo sana lakini kama wazazi tulisimama naye na kumpa kila aina ya msaada aliouhitaji kuhakikisha anaifikia ndoto yake na hapo baada ya kufika elimu ya chuo kikuu aliandika mashairi mengi ya watu tofauti tofauti wakiwamo viongozi na watu mashuhuri” Alisema Dkt. Kingu
Mbali ya kitabu hicho, Wakili Aisha ameshaandika vitabu vingine vitano ambavyo vipo sokoni na kuendelea kutoa elimu na maarifa kwa Watanzania wakiwemo vijana.
Aisha ameandika mashairi ya kumbukumbu na heshima kwa viongozi wa dunia, watu mashuhuri, taasisi mbalimbali, na masuala ya kitaifa. Baadhi ya watu na taasisi alizowahi kuzitunuku kupitia mashairi yake ni pamoja na:

Viongozi Wakuu wa Nchi Duniani: Barack Obama, Michelle Obama, Vladimir Putin, Nelson Mandela, na Jakaya Mrisho Kikwete.
Watu Mashuhuri wa Kimataifa: Queen Elizabeth II katika maadhimisho ya miaka yake 92, Prince William kutokana na juhudi zake dhidi ya ujangili, Martin Luther King Jr., Kofi Annan, pamoja na Angellah Kairuki.
Viongozi wa Kidiplomasia na Mashirika: Balozi Yuri Popov, Mkurugenzi Mtendaji wa CPTM Michaela Smith, Ruth Zaipuna, Dkt. Moses Nkundwe Mwasaga, Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Ali Mwema, na Dkt. Kingu Saidi Mtemi.
Heshima kwa Taasisi na Utamaduni: SADC 39th Summit, BBC Swahili, Taifa Stars wakati wa AFCON 2019, Serengeti Boys katika michuano ya AFCON ya vijana chini ya miaka 17, pamoja na viongozi na wasomi mbalimbali wa Nelson Mandela African Institution of Science and Technology.