Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia , Dar es Salaam
Bingwa wa dunia wa mbio ndefu, Alphonce Felix Simbu, anatarajiwa kushiriki Marathoni ya Mawakili wa Serikali itakayofanyika Mei 31, 2026 jijini Dodoma, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kutambua haki zao pamoja na kupata msaada wa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Addo November, amesema marathoni hiyo itakuwa ya kipekee kutokana na mwitikio mkubwa wa washiriki walioanza kujisajili kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amesema ada ya usajili kwa washiriki ni Sh. 40,000 huku waliolipia Sh150,000 wakitarajiwa kupatiwa zawadi ya traksuti, sambamba na medali na zawadi nyingine mbalimbali kwa washiriki na washindi wa mbio hizo.
“Sisi Mawakili wa Serikali tunafanya kazi nyingi za kisheria katika kusaidia nchi yetu kwa kushirikiana na mawakili binafsi, hivyo tunaungana pamoja kwenye marathoni hii ambapo tutaweka miili yetu sawa kwa kushiriki mbio fupi na ndefu pamoja na watoto. Wananchi nawakaribisha sana waendelee kujisajili,” amesema Wakili Addo.
Aidha amesema marathoni hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Wakili Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, huku akieleza kuwa jiji la Dodoma linatarajiwa kufurika kutokana na idadi kubwa ya washiriki.
Katika hatua nyingine, Wakili Addo amesema kupitia mbio hizo wataendelea kuhamasisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi, akibainisha kuwa Mawakili wa Serikali walishiriki kikamilifu katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign iliyowafikia zaidi ya wananchi milioni nne nchini kote.
“Katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid tuligundua kesi zinazowasumbua wananchi kwa kiwango kikubwa ni migogoro ya ndoa na ardhi,” amesema.
Kwa upande wake, mwanariadha wa zamani wa mbio za marathoni nchini, Juma Ikangaa, amewahamasisha wanawake kujitokeza kushiriki marathoni hiyo, akisema wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika mashindano ya riadha.
Amesema historia inaonyesha kuwa hata mwaka 1965 mwanamke mmoja aliwahi kushinda medali katika mashindano ya riadha, hivyo hakuna sababu ya wanawake kujiweka nyuma nyuma katika mashindano hayo.





