Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema kuwa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) hazilengi umaarufu wala thamani ya fedha, bali zinatambua ubora wa kazi, weledi na mchango wa waandishi wa habari katika kuibua masuala yenye manufaa kwa kuibadilisha jamii.

MCT imeeleza kuwa tuzo hizo zimeendelea kuwa chachu ya kuwahamasisha waandishi kuzingatia maadili ya taaluma, kufanya kazi zenye athari chanya kwa wananchi na kuendeleza uandishi wa habari wenye viwango vya juu nchini.

Akizungumza leo Mei 19, 2026 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), Ernest Sungura, ametangaza majina ya waandishi 18 walioteuliwa kuwania tuzo za EJAT msimu wa 16.

Amesema uteuzi huo umefanyika kupitia mfumo mpya wa kidigitali uliotumika kwa mara ya kwanza kuchakata jumla ya kazi 594 zilizowasilishwa na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini katika makundi 11 ya tuzo hizo, hatua inayotajwa kuongeza uwazi, usahihi na ufanisi katika mchakato mzima wa tathmini.

“Kupitia mfumo huu mpya wa kidigitali, jumla ya kazi 60 ziliondolewa katika hatua za awali baada ya kubainika kutokidhi vigezo vya msingi vya mashindano kabla ya kufikishwa kwa majaji kwani Mfumo huu umeongeza uwazi na kuondoa mianya ya upendeleo, kwani maamuzi yote yalifanyika kwa kuzingatia alama zilizopatikana pekee,” amesema Ernest Sungura.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende, amesema taasisi hiyo imeanzisha fellowship maalum ya uandishi wa habari za elimu inayolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutumia tafiti, takwimu na tathmini mbalimbali katika kuandaa habari zenye ubora na athari chanya kwa jamii.

Amesema mpango huo unakusudia kuhamasisha uandishi wa kina unaochochea mjadala wa maendeleo ya sekta ya elimu na kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kupitia taarifa zenye ushahidi na weledi wa hali ya juu.

“Fellowship hii itaendeshwa kwa kipindi cha miezi sita, ambapo waandishi wa habari watapatiwa mafunzo ya kitaaluma pamoja na uwezeshaji wa kufanya kazi kwa vitendo ili kuwajengea uwezo wa kuandaa habari za elimu zenye ubora na athari kwa jamii,” amesema Baraka Mgohamwende.

Kwa mujibu wa Uwezo Tanzania, awamu ya kwanza ya programu hiyo ilianza ikiwa na waandishi 17, lakini waandishi 12 pekee ndio waliofanikiwa kuendelea hadi hatua ya sasa ya programu hiyo inayolenga kukuza uandishi wa habari unaotumia tafiti na ushahidi wa kitaalamu.

Katika hatua nyingine, waandaaji wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) wametangaza kuwa majina ya washindi wa msimu wa 16 yatawekwa hadharani rasmi Mei 29, 2026 katika hafla maalum itakayofanyika katika ukumbi wa Four Points by Sheraton Dar es Salaam New Africa jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari huku Rais wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nestor Kayobera, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Miongoni mwa waandishi 18 walioteuliwa kuwania tuzo hizo ni Shaban Hamisi wa Nipashe, Simon Mkina wa Pambazuko Online, Daniel Samson wa Nukta Africa, Devotha Kihwelo wa Mwananchi, Abdallah Kurwa wa ITV pamoja na Joseph Kirati wa The Chanzo, huku ushindani ukitajwa kuwa mkubwa kutokana na ubora wa kazi zilizowasilishwa mwaka huu.