Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameahidi kutoa kitita cha shilingi milioni 50 kwa timu ya Basketball ya Dar City Club iwapo itaibuka na ushindi katika hatua ya robo fainali dhidi ya Petro de Luanda kwenye mashindano ya Afrika ya Basketball (BAL).
Ahadi hiyo ameitoa leo Mei 20, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akiwakabidhi bendera wachezaji wa timu hiyo wanaoelekea nchini Rwanda kwa ajili ya kuendelea na hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Chalamila amesema kuwa hatua iliyofikiwa na Dar City ni historia kubwa kwa Tanzania kwani haijawahi kutokea tangu nchi ipate Uhuru kwa timu ya ndani kufika hatua ya robo fainali katika mashindano makubwa ya Afrika ya Basketball.
“Tunajivunia mafanikio haya makubwa ya Dar City. Mmeonyesha uwezo mkubwa na mmetangaza vyema jina la Tanzania kimataifa. Mkishinda dhidi ya Petro de Luanda, nitawapatia milioni 50 kama motisha,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, nyota wa Basketball wa Tanzania Hasheem Thabeet ameishukuru Serikali pamoja na Watanzania kwa kuendelea kuwapa sapoti na morali kubwa wachezaji hao kuelekea mchezo huo muhimu.
Thabeet amesema sapoti wanayoipata kutoka kwa viongozi na wananchi inawapa nguvu zaidi ya kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania na kurejea nyumbani na ushindi.
“Ni kweli tulienda South Africa na tukapata matokeo tuliyoyatarajia, lakini bado safari yetu haijaisha. Sasa tunaelekea kwenye mchezo muhimu wa robo fainali dhidi ya timu ya Kigali, Rwanda. Tunaamini kwa uwezo wetu, tukifanikiwa hatua hii tutatinga nusu fainali na hatimaye kucheza fainali. Tunaendelea kuhitaji sapoti na hamasa yenu kubwa, kwani nguvu yenu ndiyo inayotupa morali ya kupambana zaidi. Tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa nyuma yetu katika kila hatua.”amesema Thabeet
Dar City imeondoka nchini Mei 20, 2026 kuelekea Rwanda tayari kwa maandalizi ya mchezo wa robo fainali wa mashindano ya BAL dhidi ya Petro de Luanda, huku Watanzania wengi wakionesha matumaini makubwa kwa timu hiyo kufanya vizuri na kuandika historia nyingine mpya katika mchezo wa Basketball Afrika.





