Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewasisitiza watendaji wa kata mkoani humo kuwa chachu ya kuchochea maendeleo kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato pamoja na kutatua kero za wananchi .

Kunenge alitoa msisitizo na maagizo mbalimbali wakati akizungumza na watendaji wa kata 134 kati ya 136 zilizopo mkoani Pwani,Mei 25,2026 ambapo aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili mkoa kuongeza mapato zaidi ifikapo Juni 2026.

Alieleza Mkoa huo umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato baada ya kuongezeka kutoka asilimia 87.9 mwezi Juni 2025 hadi asilimia 106 mwezi Machi 2026.

Aidha, aliwaagiza watendaji hao kuepuka kuingilia mihimili mingine, ikiwemo Mahakama na Mabaraza ya Ardhi, vinavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Kunenge alisema watendaji hawapaswi kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya mahakama, bali wanatakiwa kushughulikia migogoro ambayo bado haijafikishwa mahakamani ili kuzuia migogoro kuendelea kuongezeka.

Vilevile alibainisha wimbi la uvamizi wa ardhi unaofanywa na baadhi ya wananchi hivyo aliwahimiza watendaji kutenda haki bila kuchochea migogoro huku akisisitiza kulindwa kwa ardhi zinazomilikiwa kihalali.

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, ikiwemo kuongeza pato la Taifa, pato la mtu mmoja mmoja, kuzalisha ajira, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kukuza uwekezaji na viwanda.

Kwa mujibu wa Kunenge ,”Mkoa hauamini katika kushindwa na kwamba anahitaji kuona mabadiliko kuanzia ngazi za chini za uongozi ifikapo mwaka 2030 ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kupeleka tabasamu ya kimaendeleo kwa wananchi .

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Pangani, Benjamin Mputu aliipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwakutanisha watendaji hao ili kujadili changamoto mbalimbali na kukumbushana wajibu wao, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji katika utendaji kazi.