OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 2.7 kabla ya Aprili 2022 hadi zaidi ya asilimia 16 ya kaya hivi sasa , hatua inayotafsiriwa kuwa mafanikio ya juhudi za Serikali katika kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mafanikio hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Afisa Masoko na Uhusiano wa NBS, Andrew Punjila, wakati wa maonyesho ya kilele cha Wiki ya Mazingira yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma chini ya kaulimbiu ya “Dira 2050: Tuwajibike Kukijakisha Tanzania.”
Punjila alisema maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa taasisi mbalimbali kuonesha mchango wao katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, huku NBS ikitumia jukwaa hilo kuonesha namna takwimu rasmi zinavyosaidia kupima maendeleo ya Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo mazingira.
Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Tanzania yenye uchumi imara, mazingira salama na uhakika wa chakula, mambo ambayo yanategemeana kwa kiwango kikubwa na usimamizi mzuri wa mazingira.
“Tunataka kuona Tanzania ya kijani yenye uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa njia endelevu,Hili haliwezekani bila kulinda mazingira ambayo ndiyo msingi wa sekta nyingi za uzalishaji,” alisema.
Kwa mujibu wa Punjila, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhifadhi mazingira kutokana na umuhimu wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa sekta zinazotegemea kilimo.
Alieleza kuwa katika kutathmini mafanikio ya hatua hizo, takwimu rasmi zimekuwa nyenzo muhimu ya kupima maendeleo ya Taifa kuelekea malengo ya Dira 2050 na uchumi wa kati wa juu.
“Takwimu ndizo zinazotuonesha tumetoka wapi, tuko wapi na tunakoelekea. Zinatusaidia kupima kiwango cha maendeleo tunachokifikia katika safari ya kujenga uchumi mkubwa na shindani,” alisema.
Akitolea mfano wa mchango wa takwimu katika sekta ya mazingira, Punjila alisema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa zaidi ya asilimia 55 ya kaya nchini bado zinatumia kuni kwa ajili ya kupikia, huku zaidi ya asilimia 26 zikitumia mkaa.
Alisema hali hiyo ina maana kuwa zaidi ya asilimia 80 ya kaya nchini bado zinategemea nishati zisizo safi kwa matumizi ya kupikia, jambo linalochangia uharibifu wa mazingira na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, alisema ongezeko la matumizi ya nishati safi linaashiria kuwa juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala zinaanza kuzaa matunda.
“Matokeo haya yanaonesha kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza matumizi ya nishati safi zinaendelea kuleta mabadiliko chanya. Huu ni mchango muhimu katika kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Aliongeza kuwa NBS itaendelea kuzalisha na kusambaza takwimu rasmi zitakazosaidia watunga sera, wadau wa maendeleo na wananchi kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa.


