Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limefungua tena dirisha la kujiunga na mafunzo kwa vijana waliochaguliwa mwaka 2026 lakini wakashindwa kuripoti katika makambi waliyopangiwa awali, likiwataka kutumia fursa hiyo kwa kuripoti kwenye makambi yaliyo karibu na maeneo wanayoishi.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo June 12,2026 jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Mafunzo la JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amesema uamuzi huo umefikiwa ili kuhakikisha hakuna kijana anayekosa nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kutokana na changamoto mbalimbali zilizomzuia kuripoti kwa wakati.

Amesema vijana wote waliokosa kuripoti wanapaswa kuelekea katika Kambi ya Ruvu JKT mkoani Pwani, Kambi ya Makutupora JKT mkoani Dodoma au Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji, Dar es Salaam, kulingana na ukaribu wa eneo wanaloishi.

“Vijana wote waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT lakini hawakuripoti kutokana na sababu mbalimbali wanatakiwa kuripoti katika makambi yaliyo karibu na maeneo wanayoishi,” amesema Brigedia Jenerali Mnyani.

Amefafanua kuwa zoezi hilo la kupokea vijana hao litafanyika kuanzia Juni 12 hadi Juni 15, 2026, huku akiwahimiza kutumia nafasi hiyo kabla ya muda uliotengwa kuisha.