Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Wazazi na walezi wametakiwa kuongeza juhudi katika kuwalea watoto kwa kuzingatia maadili mema na kuwapa nafasi ya kusikilizwa, hatua ambayo imeelezwa kuwa msingi muhimu wa kuwajenga watoto wenye kujiamini, kuwajibika na kuepuka tabia hatarishi zinazoweza kuathiri mustakabali wao.

Sambamba na hilo, jamii imehimizwa kuheshimu na kulinda haki za watoto ili waweze kukua katika mazingira salama, yenye upendo na yanayowawezesha kufikia ndoto zao.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Faithmary Lukindo, alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo jijini Dodoma.

Lukindo amesema wazazi na walezi wana jukumu kubwa la kuwajenga watoto katika misingi ya maadili mema ili kuwakinga dhidi ya ushawishi wa tabia zisizofaa zinazoweza kuharibu maisha yao na kuathiri maendeleo yao ya baadaye.

Amesema mtoto anapopewa haki ya kusikilizwa na kutoa maoni yake, hujengewa hali ya kujiamini na kujiona mwenye thamani ndani ya familia na jamii inayomzunguka.

“Kumpatia mtoto haki ya kusikilizwa kwa kutoa maoni yake kunamsaidia kujiamini na kujiona mwenye thamani katika familia na hata katika jamii anayoishi. Hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwapa watoto wao fursa hiyo,” amesema.

Aidha, amesema Serikali kupitia wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza ustawi wa watoto na kuhakikisha haki zao zinazingatiwa wakati wote.

“Watoto ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa la kesho, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha wanapata malezi bora, ulinzi na mazingira rafiki yatakayowasaidia kufikia ndoto zao,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Jukwaa la Haki za Watoto Tanzania, Sylvia Ruambo, ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwalinda na kuwapenda watoto bila ubaguzi, akisisitiza kuwa watoto wote wana haki sawa zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa.

“Tunaomba jamii iendelee kuwalinda na kuwapenda watoto kwani wote wana haki sawa. Sisi kama Bodi tutakuwa mstari wa mbele kutetea na kulinda maslahi yao,” amesema.

Naye Askofu wa Kanda ya ECM Bethel, Richard Mwalyego, amesema kuanzishwa kwa mradi wa saluni katika Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha watoto kupata ujuzi wa kujitegemea na kujenga maisha bora ya baadaye.

Amefafanua kuwa kituo hicho kinaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kugusa mahitaji ya watoto na jamii kwa ujumla, huku ikiimarisha uwezo wao wa kukabiliana na changamoto za maisha.

“Mradi huu wa saluni umeanzishwa kwa lengo la kuwapatia watoto ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuwaepusha na vishawishi viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao,” amesema.

Mwalyego pia amewataka wazazi kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya maadili na imani njema ili kuwaandaa kuwa raia wema na wenye mchango chanya kwa taifa.

Kwa niaba ya Afisa Elimu Kata ya Hombolo, mwalimu aliyemwakilisha amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya elimu ili kuwasaidia watoto kutimiza ndoto zao na kufikia malengo waliyojiwekea.

Ameongeza kuwa walimu wana wajibu wa kuongeza bidii katika kuwafundisha na kuwaongoza watoto ili waweze kufanikiwa katika masomo na maisha yao kwa ujumla.

“Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha watoto wanatimiza ndoto zao. Sisi walimu tuna wajibu wa kuongeza juhudi ili kuwasaidia kufikia malengo yao na kuwa raia bora wa baadaye,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo cha Malezi ya Watoto Kikombo, Darius Kalijongo, amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali za kitabia kutokana na watoto wanaotoka katika mazingira tofauti ya kijamii.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, kituo kimeimarisha mifumo ya uangalizi ikiwemo uwekaji wa kamera za usalama katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuzuia vitendo viovu na kuimarisha malezi.

“Changamoto za kitabia ni miongoni mwa changamoto kubwa tunazokabiliana nazo. Ndiyo maana tumeimarisha mifumo ya uangalizi ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye kuwajenga,” amesema.

Kalijongo ameongeza kuwa kituo hicho kinaendesha miradi mbalimbali ya uzalishaji ambayo imekuwa ikichangia upatikanaji wa chakula na kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa hapo.