Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa asilimia 97.66 baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndio kuunga mkono Bajeti hiyo

Akitangaza matokeo ya kura ya wazi iliyopigwa bungeni jijini Dodoma, Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu alisema kuwa kati ya kura hizo 393 zilizopigwa, kura 8 zimekataa kuunga mkono bajeti hiyo na wabunge wengine nane 8 hawakupiga kura kwa sababu hawakuwepo bungeni.

Akihitimisha hoja baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria kwa ajili ya kuidhinisha Serikali kuanza kutekeleza Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/2026 (zaidi ya shilingi trlilioni 62.33) kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina, Mhe. Spika Zungu alimpongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Ballozi Khamis Mussa Omar (Mb) wasaidizi wake, watendaji wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya na Wabunge wote kwa michango yao yenye tija kwa Taifa.

“Kura zimepigwa na Serikali imeruhusiwa kuzitumia pesa kuanzia sasa, mkazitumie pesa hizi kama Kamati za Bunge zilivyoelekeza, kuhakikisha maslahi ya watu kwanza yanazingatiwa kabla ya mambo mengine. Bunge hili litaendelea kufuatilia utekelezaji wake na kuhakikisha kuwa miradi yote iliyoainishwa inazingatiwa na kuleta furaha kwa wananchi” alisisitiza Mhe. Zungu.

Kupitia kwa Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Serikali ililiomba Bunge lipitishe Bajeti ya shilingi trilioni 62.33 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, mapato yalitarajiwa kuwa shilingi trilioni 46.79 ambapo mapato ya kodi ni shilingi trilioni 36.99, mapato mengine ni shilingi trilioni 9.24 (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.977) na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi bilioni 563.1.

Aidha aliongeza kuwa ili kuendana na dhamira ya kujitegemea katika uendeshaji wa Serikali na maendeleo, takribani robo tatu ya bajeti yote ya mwaka 2026/27, sawa na asilimia 74.2 itagharamiwa na mapato ya ndani.

Matumizi na uwekezaji katika mali zisizo za kifedha yalikadiriwa kuwa shilingi trilioni 54.50 pasipo kujumuisha malipo ya mtaji wa deni la Serikali ambapo kati ya kiasi hicho, stahiki za watumishi ikijumuisha michango ya pensheni ni shilingi trilioni 10.13.

“Gharama za bidhaa na huduma itakuwa shilingi trilioni 5.22, malipo ya riba ni shilingi trilioni 6.86, ruzuku shilingi trilioni 25.32, mafao na misaada ya kijamii shilingi trilioni 1.01, uwekezaji katika mali zisizo za kifedha shilingi trilioni 2.33 na gharama nyingine shilingi trilioni 3.63.” alisema Mhe. Balozi Omar

Aliongeza kuwa kulingana na makadirio ya mapato na matumizi hayo, kunajitokeza nakisi kwenye bajeti ya shilingi trilioni 7.71 na Serikali itaendelea kugharamia nakisi ya bajeti hiyo kwa kutumia mikopo kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa kuzingatia Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni la Serikali (2025/26 – 2027/28).

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, katika mwaka 2026/27, Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni 15.54 ambapo kati ya kiasi hicho, mikopo ya ndani itakuwa shilingi trilioni 6.56, mikopo ya nje yenye masharti nafuu shilingi trilioni 6.55 na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 2.43.

Aidha, Serikali inakadiria kulipa malipo ya mtaji kwa mikopo iliyoiva shilingi trilioni 7.84.

Baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Bunge linatarajia kupokea, kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2026 ( The Finance Bill,2026) tarehe 24 Juni, 2026.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na Naibu Mawaziri wake, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na Mhe. Laurent Luswetula (Mb) wakipongezwa na Wabunge mbalimbali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya wabunge hao kupitisha kwa kishindo makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya shilingi Trilioni 62.33 kwa mwaka 2026/2027, ambapo zaidi ya wabunge 385 sawa na asilimia 97.66 walipitisha kwa kura za ndio.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakipongezana baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa asilimia 97.66 baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndio kuunga mkono Bajeti hiyo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akipongezwa na Wafanyakazi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mzigu ya mkoani Mwanza, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa asilimia 97.66 baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndio kuunga mkono Bajeti hiyo.
Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kushoto) na Bw. Joshua Nsubili, wakipongezana baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa asilimia 97.66 baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndio kuunga mkono Bajeti hiyo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango na Uwekezaji, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa asilimia 97.66 baada ya wabunge 385 kupiga kura ya ndio kuunga mkono Bajeti hiyo.