Na Prosper Makene
Geneva – Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva ametoa wito wa kuwa na mifumo ya mali miliki (Intellectual Property) inayojumuisha wote, yenye usawa na inayolenga mustakabali ili kuchochea ubunifu na maendeleo endelevu.
Akizungumza katika Mkutano wa 68 wa Mabaraza ya Nchi Wanachama wa Shirika la Kimataifa la Mali Miliki WIPO, Balozi Temu aliwashukuru Mwenyekiti na Makamishna wenzake kwa uongozi wao. Pia alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Bw. Daren Tang, kwa kuteuliwa tena na kuipongeza Sekretarieti kwa maandalizi bora ya mkutano huo. Tanzania iliungana na tamko lililosomwa na Afrika Kusini kwa niaba ya Nchi za Afrika na Nepal kwa niaba ya Nchi Zinazoendelea.
Balozi Temu, ambaye alikuwa anamwakilisha Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa Geneva, Mhe. Dkt. Abdallah S. Possi, alisema Tanzania inatambua mali miliki kama kichocheo muhimu cha ubunifu, viwanda na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Katika uchumi unaotegemea maarifa, alibainisha kuwa akili mnemba ina uwezo mkubwa wa kubadilisha na kuharakisha ubunifu pamoja na ukuaji wa uchumi.
Alisisitiza kuwa mifumo jumuishi ya mali miliki, ujenzi wa uwezo na uhamishaji wa teknolojia ni muhimu ili kuwezesha nchi zinazoendelea kunufaika na akili mnemba na teknolojia nyingine mpya zinazojitokeza.
Waliomambatana na Balozi Temu katika Mkutano huo ni Bw. Godfrey Simango Nyaisa, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA; Bw. Khamis Juma Khamis, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali BPRA; na Bi. Loy Nabeta, Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Benki ya Dunia Tanzania. Uwepo wao umeonyesha dhamira thabiti ya Tanzania katika kuendeleza masuala ya mali miliki na ushirikishaji wa wadau.
Ujumbe wa Tanzania uliishukuru WIPO kwa msaada wake wa kiufundi na ujenzi wa uwezo unaoendelea nchini.
Maeneo muhimu ya msaada huo ni pamoja na Kliniki ya Usimamizi wa Mali Miliki kwa Biashara Ndogo na Waanzilishi, uanzishwaji wa Taasisi ya Mafunzo ya WIPO nchini, na miradi ya kurahisisha uhamishaji wa teknolojia kupitia vyuo vikuu na taasisi za utafiti.
Vilevile, msaada unajumuisha mafunzo ya utekelezaji wa sheria za mali miliki, Mradi wa Usimamizi wa Kielektroniki wa Taarifa, usakinishaji wa mfumo wa IPAS 4 Zanzibar, pamoja na ujenzi wa uwezo katika upimaji wa hati miliki na elimu ya mali miliki.
Balozi Temu alielezea dhamira ya Tanzania ya kuimarisha mfumo wake wa mali miliki kupitia mabadiliko ya sheria, uboreshaji wa utoaji wa huduma, utekelezaji madhubuti wa sheria, ujenzi wa uwezo wa taasisi na uhamasishaji kwa umma.
Alisema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha kuwa mali miliki inachangia ipasavyo katika ubunifu, uwekezaji, ujasiriamali, uundaji wa ajira na ukuaji wa uchumi endelevu.
Kwa kumalizia, Balozi Temu alirudia dhamira ya Tanzania ya kushirikiana kwa karibu na WIPO na Nchi Zote Wanachama.
Lengo ni kukuza mfumo wa kimataifa wa mali miliki unaounga mkono ubunifu na ustawi wa pamoja. Alivitakia mafanikio Mabaraza katika majadiliano yao.


