Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesisitiza umuhimu wa kuuenzi na kuuheshimu Muungano wa Tanzania, akieleza kuwa ni tunu ya taifa isiyopaswa kuchezewa.
Masauni ameeleza, Muungano ndio msingi wa umoja na maendeleo ya Taifa, hivyo Watanzania wanapaswa kuuenzi na kujivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano huo.
Akizungumza Chalinze, wilayani Bagamoyo, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani, Julai 22,2026 Masauni amepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayochochea shughuli za kiuchumi kati ya Bagamoyo na Zanzibar.
“Ni utashi wa Mwenyezi Mungu kuunda Muungano huu wa pande hizi mbili, sisi ni wamoja na tunaendelea kupiga hatua za maendeleo kwa kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii, uvuvi na matumizi ya rasilimali za fukwe,” anasema Masauni.
Aidha, Masauni aliwaasa vijana kupuuza baadhi ya taarifa zinazopotosha kuhusu masuala mbalimbali yaliyoasisiwa na waasisi wetu, huku akiwahimiza kutumia mitandao ya kijamii kwa tija.
Kuhusu Mazingira, aliwahimiza wananchi kuendelea kupanda miti na kuacha ukataji hovyo wa miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika ziara hiyo, Masauni amezindua greda la kuchonga barabara Chalinze, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Msoga unaotarajiwa kugharimu Sh bilioni 2.2, na madarasa nane pamoja na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Chalinze wenye thamani ya Sh milioni 182.9, zinazotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Ridhiwani Kikwete, alieleza Halmashauri ya Chalinze imeendelea kupiga hatua za maendeleo kutokana na ongezeko la mapato ya ndani kila mwaka.
Akizungumzia uzinduzi wa greda hilo, Ridhiwani alieleza litasaidia kuokoa muda na gharama zilizokuwa zikitumika kuboresha miundombinu ya barabara za ndani, hivyo fedha hizo sasa zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuufungua mji wa Bagamoyo kiuchumi, akieleza kuwa zaidi ya Sh bilioni 27 zilitolewa mwaka uliopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alifafanua maboresho ya miundombinu ya barabara na reli yameongeza mvuto wa uwekezaji katika wilaya ya Bagamoyo.
Alieleza utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Bandari ya Bagamoyo, barabara ya Makofia–Mzenga hadi Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa kiwango cha lami, pamoja na fursa zilizopo katika sekta za utalii na uvuvi, utaendelea kufungua milango ya ukuaji wa uchumi.
Kunenge ameongeza kuwa ili Mkoa wa Pwani uendelee kunufaika na mageuzi ya kiuchumi, kuna haja ya kuhamasisha uwekezaji wa hoteli kubwa na za kisasa zitakazovutia wawekezaji na watalii wengi zaidi.
Mkuu huyo wa Mkoa amemuomba Waziri Masauni kufikisha ombi la Halmashauri ya Chalinze kuwa Manispaa kutokana na kuwa na vigezo vingi kikiwemo cha ongezeko la kukua kwa mapato.











