Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Suala la ulinzi ,amani na usalama wa taifa limeelezwa kuwa sababu kuu iliyosababisha Serikali kusitisha kwa muda mikutano ya hadhara nchini, huku ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni ya muda na itafutwa mara tu vyombo vya dola vitakapojiridhisha kuwa hakuna tena viashiria wala vihatarishi vya usalama wa wananchi na mali zao.
Msimamo huo umetolewa leo July 22,2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake katika Soko la Machinga na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma.
Msigwa amesema taarifa za kiintelijensia kutoka vyombo vya ulinzi na usalama zilionesha kuwepo kwa mipango ya baadhi ya watu wenye nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi, jambo lililoifanya Serikali kuchukua hatua za tahadhari ili kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Amesisitiza kuwa jukumu la msingi la Serikali ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa wakati wote, akibainisha kuwa Tanzania ina vyombo imara vya ulinzi na usalama vyenye wajibu wa kutambua na kudhibiti vihatarishi kabla havijageuka kuwa migogoro.
“Polisi walibaini kuwepo kwa mipango ya watu wenye nia ovu. Serikali ina wajibu wa kulinda raia na mali zao. Hii ni nchi yenye misingi ya kikatiba, lakini tunapolinda usalama wa wananchi hakuna mzaha ikikatazwa, imekatazwa, mpaka tutakapojiridhisha” amesema Msigwa.
Msigwa amekumbushia matukio ya kiusalama yaliyotokea Oktoba 29 mwaka jana kuwa yalisababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha kwa baadhi ya wananchi na hasara za mali, hivyo Serikali haitakuwa tayari kuona hali kama hiyo ikijirudia.
“Hatutaruhusu yaliyotokea mwaka jana yajirudie tena. Watu walipoteza maisha na Watanzania walipata hasara. Never and never again,” amesisitiza.


