Na Florid Mapunda, Mtwara
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliundwa kwa malengo ya kuboresha ushirikiano kati ya nchi huru wanachama, kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi hizo na kukuza biashara baina yao ili uhuru uwe na maana kwa wananchi wa nchi hizo.
SADC ambayo ni (Southern African Development Community) ilianzishwa mwaka 1992 na wananchama wake wa sasa ni Angola, Botswana, DR Congo, na Lesotho.
Wanachama wengine kwenye Jumuiya hii ni Madagascar, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Afrika Kusini, Eswatini, Tanzania, Zambia and Zimbabwe.
Uhuru una sura mbili: sura ya kwanza ni uhuru wa bendera na sura ya pili ni uhuru wa uchumi. Uhuru wa uchumi unahusisha pia mambo mawili: kwanza kuzalisha bidhaa za kutumia ndani na za kuuza nje.
Pili ni uwezo wa kununua bidhaa za nje kwa mahitaji ya wananchi na kwa ajili ya maendeleo yao.
Katika kutimiza azma ya SADC ya kukuza biashara baina ya nchi wanachama, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ilifungua milango kwa nchi wanachama wa SADC kutumia Bandari ya Mtwara kuingiza bidhaa na kusafirisha nje bidhaa zao kwa ajili ya maendeleo.
Uamuzi huu wa kuhudumia nchi za SADC zenye uhitaji uliitwisha Bandari ya Mtwara jukumu zito na kusababisha maboresho ya kuifanya Bandari ya Mtwara iwe ya kisasa na ifanye kazi kwa ufanisi.
Maboresho hayo lengo lake ni kuteka sehemu ya soko la SADC ili nchi zitakazohudumiwa zinufaike na utendaji wenye ufanisi ndani ya Bandari ya Mtwara. Kwa mfano sasa bandari hii inaweza kuhudumia meli nne ndani ya wiki moja.

Serikali imekusudia kuboresha miundombinu ya barabara na reli. Kadiri miundombinu itakavyoboreka biashara ndani ya Malawi itashamiri na kufanyika kwa faida. Na kuna uwezekano wafanyabiashara wa Zambia na kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakawa wanatumia hii ya Bandari ya Mtwara.
Bandari ya Mtwara pia inahudumia nchi za nje zikiwemo India na Comoro na visiwa vya Shelisheli.
Lakini bandari hii inatarajiwa kukuza biashara na kuchochea maendeleo ndani ya Tanzania, na hasa kusini mwa Tanzania. Ni kwa sababu hii TPA imeendeleza maboresha katika bandari hii kutokana na umuhimu wake katika kuhudumia mikoa ya kusini mwa Tanzania. Mikoa hiyo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Songwe na Mbeya.
Mikoa ya kusini mwa Tanzania ni mikoa muhimu katika kuzalisha mazao ya chakula na inachangia sehemu kubwa katika kulifanya taifa lijitegemee kwa chakula. Lakini mikoa hii pia inazalisha mazao ya biashara yanayouzwa nje. Kwa mfano njegere, kahawa, maparachichi ni mazao yanayozalishwa katika mikoa hiyo na kuuzwa nje.
Kazi kubwa inayoukabili uongozi wa mikoa hiyo na vyama vya ushirika na kuhakikisha wakulima wanaweka katika soko mazao yenye sifa. Kuuza mazao machanga au yenye kasoro ni kulidhuru soko la ndani na la nje. Waingereza wana msemo wao kwamba ubora unakuhakikishia soko na mafanikio ya baadaye.
Suala la ubora lazima lizingatiwe sana kulima, kuvuna na kutunza mazao kabla ya kuyaweka sokoni. Kupuuza ukweli huu ni kuharibu soko la mazao ya Tanzania na kwa hiyo kudhuru jitihada inayofanywa na serikali na taasisi zake kitika kuinua maendeleo ya taifa.
Maboresho ambayo yamefanywa na TPA kwa lengo la kuinua maendeleo ya Taifa ni yapi?
Tukipima maboresho yaliyofanywa katika kipindi kinachoishia katikati ya Julai 2026, tunagundua kwamba TPA imeongeza gati moja yenye urefu wa mita 300 na kuifanya bandari hii iwe na gati mbili zenye urefu wa jumla ya mita 685.
Kwani hapo nyuma bandari ilikuwa na gati moja yenye urefu wa mita 385. Kutokana na maboresho hayo meli kubwa na ndogo sasa zinaweza kutia kutia nanga, kushusha na kupakia mizigo kwa wakati mmoja.
Aidha TPA imefanikiwa kujenga eneo la kuhifadhi mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 159,000 wakati eneo la awali lilikuwa na mita za mraba 38,000. Eneo la sasa linaweza kuhifadhi hadi tani milioni 1.7 kwa mwaka. Maboresho haya yanaiwezesha bandari ya Mtwara kuhudumia takribani tani milioni moja za mizigo kwa mwaka kitu abacho hapo mwanzo haikuwa rahisi.
Katika maboresho hayo, Mamlaka imeongeza vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyotumika bandarini hapo. Vifaa hivyo ni pamoja na kreni zitembeazo zinazohitajika sana katika kushusha na kupakia mizigo. Kadhalika zimenunuliwa kreni maalumu zinazoitwa ship-to-shore gantry crane, matrekta na vifaa vingine mbalimbali vya kuhudumu ndani ya bandari na kunyanyua ufanisi.
Waswahili wana msemo wao kwamba: Chema chajiuza, kibaya chajitembeza. Ni ubora wa sasa wa Bandari ya Mtwara unaoifanya Malawi ichague kutumia bandari hii katika kuingiza na kuuza bidhaa zake nje.
Bandari hii kama taasisi ya kiuchumi inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi. Kwa mfano wakati wa ujenzi wa miradi watu huajiriwa kwa muda, kuwepo kwa taasisi hii kunatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kufanya biashara tofauti tofauti kama ya chakula, maji na vinywaji baridi.

Fursa nyingine za ajira kudumu ambazo hazijitokezi moja kwa moja ni kama nyumba za wageni ambao hufanya kazi za muda bandarini au wanatumia bamdari na kuondoka.
Fursa kama hizi za kiuchumi na kijamii zinaleta utulivu katika jamii (social harmony) kwa sababu zinapunguza ugumu wa maisha hasa kwa wananchi wanaoishi jirani na bandari.
Mtu anapotembelea Bandari ya Mtwara hakosi kusikia misemo ya utani kama Mtwara kuchele, msemo wenye maana ya kwamba Mtwara kuzuri: eti kwa sababu ya maendeleo ya sasa, Mtwara kunapendeza, kumewavuta watu wengi mbali ya wazaliwa wa mikoa ya kusini.
Juma lililopita wataalamu wa masuala ya nishati kutoka Malawi walitembelea bandari hiyo na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa maboresho makubwa yaliyofanywa hasa katika miundombinu ya kuhudumia shehena ya mafuta.
Wataalamu hao walivutiwa hasa mfumo mzuri wa kushusha na kupakia mafuta ambayo yanasaafirishwa mpaka nchini Malawi na nchi nyingine. Upatikaji wa mafuta siku hizi ni tatizo kubwa kutokana na Marekani kuishambulia Iran. Vita hivyo vimevuruga uzalishaji na usafirishaji wa mafuta duniani yanayozalishwa katika eneo la Guba ya Uajemi.
Ujumbe uliotembelea Bandari ya Mtwara uliongozwa na Mtaalam wa Masuala ya Udhibiti wa Uchumi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Malawi (Malawi Energy Regulatory Authority – MERA), Bw. Alex Calvin Banda. Bw Banda alisema kuwa ubora wa bandari ya Mtwara ni darasa zuri kwao kwani wamepata ujuzi wa namna bora ya kuhudumia bandari zao za ziwa Nyasa.
“Kupitia ziara hii, tumejifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mnyororo mzima wa huduma za shehena ya mafuta katika Bandari ya Mtwara: kuanzia meli zinapowasili bandarini, upakuaji wa mafuta, uhifadhi wake katika matanki yanayomilikiwa na kampuni za sekta binafsi, hadi upakiaji katika malori yanayosafirisha mafuta kwenda katika nchi mbalimbali, ikiwemo Malawi”, alisema Bw Banda.
Ilielezwa kwamba wadau wa Malawi hunufaika zaidi wanapotumia Bandari ya Mtwara, kuliko wanapotumia Bandari za Dar es Salaam na Beira ya Msumbiji.
Ilielezwa kwamba hii siyo mara ya kwanza kwa Bandari ya Mtwara kupokea wageni wa kubadilishana nao uzoetu. Ujumbe wa aina hii kutoka nchini Kongo (DRC) nao umetembelea Bandari ya Mtwara kwa madhumuni ya aina hiyo.
Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alieleza kwamba maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanya yameongeza uwezo wa njia za kupokea na kusukuma mafuta kwenda kwenye matanki ya kuhifadhia, hatua ambayo imeongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja.
Alieleza kuwa maboresho yamefanywa kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kwamba ushirikiano huo ukifanywa kwa weledi unatoka mazuri na yenye faida kwa taifa.
Ilielezwa kwamba maboresho ya ujenzi wa Bandari ya Mtwara yameifanya bandari “kuwa na ubora usiomithilika ambao kwa kawaida ni nadra kuukuta katika bandari za kiafrika.”
“Tumeridhishwa sana na maboresho ya mfumo wa kupokea, kupima na kusukuma mafuta (Flow Metre), teknolojia hiyo imeongeza uwezo wa Bandari ya hii kuhudumia shehena kubwa za mafuta kwa ufanisi zaidi”, ilielezwa, na ikaongezwa kwamba mtiririko huo unazuia udanganyifu unaofanywa na madereva wa malori katika kuficha upotevu wa mafuta. Kwa mfumo unaotumiwa na Bandari ya Mtwara sasa takwimu zote zinasafirishwa kwa njia ya mtandao mpaka mzigo unapofika kwa mteja.
Bandari ya Mtwara imeendelea kuimarisha nafasi yake kama lango muhimu la biashara ya kikanda baada ya kuhudumia meli 4 ndani ya wiki moja na kushusha zaidi ya magari makubwa 1,500. Ni uimarishaji wa nafasi hii unaifanya bandari hii iwanie kuteka soko kubwa zaidi ndani ya SADC siku zijazo.

Magari hayo yanahudumia soko la ndani pamoja na mengine kusafirishwa kwenda nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia na Malawi kupitia Ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor), hatua inayoendelea kuongeza imani ya wafanyabiashara wa ndani na kimataifa ya kutumia bandari hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Banki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka 2021/2022, Bandari ya Mtwara ilipitisha shehena ya tani 592,400. Taarifa ya BoT ya mwaka 2024/2025 inaonyesha kuwa bandari ilipitasha tani 2,577,300. Kwa maana hiyo katika kipindi cha miaka mitatu nguvu ya bandari katika kupitisha shehena imekua mara nne.
Tija nyingine ya bandari hii ambayo imejificha kidogo ni uimarishaji wa Muugano na kuwafaidisha wananchi wa pande mbili za Muungano. Wananchi wa pande mbili za Muungano wanaitumia bandari bila kuulizwa maswali. Pengine bila Muungano wananchi wa Zanzibar wangeulizwa maswali wakati wa kutumia bandari hii.
Tanzania ni nchi ya kilimo. Kama ilivyoelezwa katika aya zilizotangulia, bandari hii imeonyesha nafasi na umuhimu wake ya kuinua kilimo kusini mwa Tanzania. Lakini bandari hii iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi na faida za kuwa katika ufukwe huu zimeonekana wazi wazi kwa wadau wa ndani na nje ya Tanzania.
Kwa hivyo Serikali ina kila sababu ya kuendeleza bandari zilizo katika ufukwe huu kama vile Bandari za Bagamoyo, Kilwa na Lindi ili kuipunguzia mzigo bandari ya Dar es Salaam na pia kusambaza neema za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo haya matatu ya pwani.


