Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema ni wakati wa kubadili mawazo kuwa miradi inayovutia wawekezaji
Hayo ameyasema katika mkutano wa Africa50 na Jukwaa la miundo mbinu Afrika uliofanyika katika ukumbi wa mwalimu Nyerere (JNICC) Jiji
Amesema mkutano ni muhimu kwani tangu kuanzishwa kwake, jukwaa hilol lmekuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi barani Afrika katika kuunda ajenda ya maendeleo ya miundombinu na uwekezaji wa bara letu.
‘Tunajivunia na kuheshimiwa sana kwamba, baada ya mafanikio ya nchi nyingine za Afrika kuandaa mikutano hii hapo awali, ikiwemo mkutano uliopita uliofanyika nchini Msumbiji, Tanzania imepewa heshima ya kuwakaribisha washiriki hawa mashuhuri mwaka huu’Amesema.

Amesema kuongezeka kwa imani ya Jumuiya ya Kimataifa na ya Afrika katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania, uwezo wake mkubwa wa kuvutia uwekezaji, pamoja na nafasi yake ya kimkakati kama lango linalounganisha masoko ya Afrika.
‘Muhimu zaidi, inathibitisha tena imani yetu ya pamoja kwamba mustakabali wa Afrika unapaswa kuongozwa na uongozi wa Waafrika, mtaji wa Waafrika, na ushirikiano wa Waafrika wenyewe.
Kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu isemayo, “Muongo wa Athari: Kutoka Kwenye Dira Hadi Utekelezaji” imekuja kwa wakati muafaka na ina umuhimu mkubwa kwetu.
Ni wazi kwamba Afrika haijawahi kukosa maono. Kupitia Ajenda ya Afrika 2063, Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), pamoja na mipango yetu ya maendeleo ya kitaifa, tumejiwekea malengo makubwa ya kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi katika jamii zetu.
Hata hivyo, kipaumbele chetu sasa kimehamia kwenye utekelezaji na narudia, utekelezaji.
Bila shaka, wananchi wetu hawapimi maendeleo kwa matamko tunayotoa, bali kwa matokeo yanayoonekana. Matokeo hayo ni pamoja na barabara bora, nishati ya uhakika, bandari na reli zenye ufanisi, miundombinu ya mawasiliano ya kidijitali, na miradi ya miundombinu inayozalisha ajira, kuvutia uwekezaji, na kuboresha maisha ya wananc
Amesema kongamano hilo lina umuhimu wa kipekee, limewakutanisha viongozi, wawekezaji, taasisi za kifedha, na washirika wa maendeleo wakiwa na lengo moja la pamoja—kubadilisha mawazo kuwa miradi inayovutia uwekezaji.

Kubadilisha ushirikiano kuwa uwekezaji halisi, na kugeuza uwezo mkubwa wa Afrika kuwa ustawi wa kudumu kwa wananchi.
‘Tunakutana katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na hali kubwa ya kutokuwa na uhakika, inayochangiwa na mvutano wa kisiasa wa kimataifa, migogoro, mabadiliko ya tabianchi, kuvurugika kwa minyororo ya ugavi, pamoja na shinikizo la kifedha.
Ingawa changamoto nyingi zimeanzia nje ya Afrika, athari zake zimeenea na kuligusa bara letu kwa kiwango kikubwa.
Hali hii inasisitiza umuhimu wa Afrika kujenga uchumi wenye uwezo wa kustahimili misukosuko na kujitegemea, kwa kuongeza thamani ya rasilimali zetu,
Kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, kupanua biashara ndani ya Afrika, na kuhamasisha mtaji wa ndani kwa ajili ya maendeleo yetu wenyewe.
Kiini cha mageuzi haya ni miundombinu, Barabara zetu, bandari, reli, mifumo ya nishati, na mitandao ya kidijitali lazima iwe chachu ya ukuaji wa uchumi, iwe na uwezo wa kustahimili misukosuko ya baadaye, na iongeze ushindani wa Afrika katika uchumi wa dunia.’Amesema
Amesema kwa upande wetu Tanzania, mageuzi ya miundombinu yanaongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo itaongoza maendeleo yetu katika kipindi cha miaka 25 ijayo.
Ambapo utekelezaji wa dira hiyo ulianza mwezi uliopita, Julai mwaka huu dira hiyo inaeleza azma yetu ya kujenga uchumi wenye ushindani, wa viwanda na shirikishi, unao endeshwa na ubunifu, rasilimali watu yenye ujuzi, maendeleo endelevu, pamoja na miundombinu ya kisasa.

Kwa kutambua kwamba mageuzi haya hayawezi kufikiwa na serikali pekee, safari yetu ya miaka 25 kuelekea mwaka 2050 imeiweka sekta binafsi katika nafasi ya msingi ya kukuza uchumi.
Ambapo Dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya mchango katika uchumi inatokana na sekta binafsi, ikiwemo wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Kwa hiyo, jukumu la Serikali ni kujenga mazingira thabiti na yanayotabirika kwa uwekezaji, kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ya umma, na kujenga ushirikiano utakaowezesha sekta binafsi kuleta mtaji, ubunifu na ujasiriamali.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imetekeleza mojawapo ya programu kubwa zaidi za maendeleo ya miundombinu katika historia yake.
Tumeipanua na kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam, jambo ambalo limeongeza ufanisi wake na kuimarisha nafasi yake kama kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda huu.
Pia tunaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), ili kuboresha muunganiko wa usafiri, kupunguza gharama za usafirishaji, na kurahisisha biashara na nchi jirani.
Vilevile, tunawekeza katika mtandao wa barabara za kimkakati, madaraja, korido za usafirishaji na vifaa vya usafirishaji, pamoja na viwanja vya ndege vya kisasa, kwa lengo la kuimarisha muunganiko wa kitaifa, kikanda na kimataifa.
Uwekezaji huu tayari umeanza kuzaa matunda kwa kupunguza gharama za usafirishaji na usafirishaji wa mizigo, pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Huenda baadaye, wakati Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre – TIC) kitakapowasilisha taarifa yake, tutaona kwa takwimu jinsi Tanzania inavyoendelea kupokea ongezeko la uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (Foreign Direct Investment – FDI).

Kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika mwambao wa Bahari ya Hindi, Tanzania imekuwa kwa muda mrefu lango la asili la kuingia Afrika.
Leo hii, kupitia uwekezaji endelevu katika miundombinu, tunaendelea kuimarisha nafasi hiyo kwa kuunganisha masoko, kurahisisha biashara, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Kama mwanachama hai wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kuwa daraja linalounganisha kanda hizi mbili muhimu.
Tumejizatiti kutumia nafasi hiyo kuimarisha biashara ya kuvuka mipaka, kuendeleza minyororo ya thamani ya kikanda, na kuvutia uwekezaji unaoleta ustawi wa pamoja.
Aidha, Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) linaimarisha juhudi hizi za kikanda kwa kuongeza biashara, uwekezaji na muunganiko wa miundombinu.
Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana kwa karibu na Africa50, serikali mbalimbali, wawekezaji na washirika wa maendeleo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayowaunganisha wananchi wetu, sekta za uzalishaji na kufungua uwezo mkubwa wa kiuchumi wa Afrika.’Amesema
Amesema wanapo zungumzia ujenzi wa kizazi kijacho cha miundombinu ya Afrika, tunazingatia zaidi kujenga mifumo iliyounganishwa ambayo itachochea maendeleo ya viwanda, ubunifu na ushindani.
Katika muktadha huo, nishati ndiyo msingi wa mageuzi ya kiuchumi. bila nishati ya uhakika, yenye gharama nafuu na endelevu, viwanda haviwezi kukua, biashara haziwezi kupanuka, na uchumi hauwezi kushindana katika soko la kimataifa.
Kwa kuzingatia ukweli huo, Tanzania inaendelea kuwekeza katika sekta ya nishati iliyo salama na yenye vyanzo mbalimbali kupitia umeme wa maji, nishati jadidifu, na gesi asilia.
Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydropower Project), pamoja na uwekezaji katika vyanzo vingine vya nishati safi, unaimarisha usalama wa nishati nchini na kuchochea maendeleo ya viwanda.
Pia tunatambua kwamba mustakabali wa nishati barani Afrika unategemea ushirikiano madhubuti wa kikanda, ujenzi wa mitandao ya kusafirisha umeme inayounganisha nchi mbalimbali, pamoja na masoko ya pamoja ya umeme ya kikanda.
Mifumo hiyo itaongeza usalama wa nishati, kupunguza gharama, na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya kukuza uchumi wetu unaoendelea kukua.
Jambo jingine lenye umuhimu sawa ni miundombinu ya kidijitali. Katika dunia ya leo, mawasiliano na muunganiko wa kidijitali ni muhimu kama ilivyo barabara, bandari na nishati.
Kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone), Tanzania inaendelea kupanua huduma za mawasiliano ya kidijitali, kuboresha utoaji wa huduma za umma, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuhamasisha ubunifu, na kuunda fursa mpya, hususan kwa vijana wajasiriamali
Kwa kuwekeza katika elimu, ujuzi wa kitaalamu, na uwezo wa kidijitali, tunaweza kuwawezesha vijana wetu kuwa wabunifu, wavumbuzi, na nguvu kuu ya kuleta mageuzi ya Afrika.
Tunaweza kuwajenga ili wasiwe watumiaji tu wa suluhisho zinazozalishwa duniani, bali wawe wazalishaji wa suluhisho zitakazoinufaisha dunia nzima.
Kama ilivyobainishwa na wazungumzaji waliotangulia, upatikanaji wa mitaji na rasilimali za kifedha kwa ajili ya uwekezaji bado ni moja ya vikwazo vikubwa vinavyozuia mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.
Hata hivyo, hali hiyo inawakilisha mojawapo ya fursa kubwa zaidi za uwekezaji kwa sekta binafsi katika kipindi hiki.
Kwa ni Serikali pekee haziwezi kugharamia utekelezaji wa matarajio makubwa ya Afrika katika maendeleo ya miundombinu.
Ni lazima tuimarishe ushirikiano unaounganisha rasilimali za serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha za maendeleo, pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Kwa hiyo, ninazialika taasisi za kifedha kushirikiana nasi, Tanzania, na kuchunguza fursa nyingi zilizopo katika sekta za usafirishaji, nishati, huduma za ugavi na usafirishaji (logistics), viwanda, miundombinu ya kidijitali, pamoja na maendeleo ya viwanda.
Tanzania siyo tena nchi inayojulikana kwa kuzalisha na kuuza malighafi pekee. Inazidi kuwa kitovu cha uwekezaji katika uongezaji thamani wa bidhaa, ubunifu, uzalishaji wa viwandani, na ukuaji endelevu wa uchumi.
Ni lazima tubadilishe dhamira zetu kuwa miradi halisi, matarajio yetu kuwa mafanikio yanayoonekana, na mipango yetu kuwa matokeo yanayopimika.
Miundombinu tunayojenga inapaswa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kupanua biashara kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), na kuunda fursa za kiuchumi kwa mamilioni ya Waafrika.
Kwa taasisi ya Africa50, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wenu na mchango wenu mkubwa katika kuendeleza mageuzi ya miundombinu barani Afrika.
Mafanikio yenu yanaonyesha wazi uwezo wa taasisi za uwekezaji za Afrika katika kutekeleza miradi yenye athari chanya na ya kudumu kwa maendeleo ya bara letu.
Mnapoanza muongo wenu mpya wa shughuli, tunawahimiza muendelee kuongoza katika kuibua suluhisho bunifu na kuhamasisha uwekezaji unaounganisha bara letu na kuboresha maisha ya wananchi wetu.
Tanzania iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Africa50. Kama mlivyoshuhudia hapa leo, tumesaini hati tatu za makubaliano ya ushirikiano (Memoranda of Understanding – MoUs) na Africa50,
Tunatarajia kuona utekelezaji wake ukiwa wa haraka, wenye ufanisi, na wenye matokeo makubwa kwa maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwa upande mwingine Rais amewahimiza kuongeza muda wa kushirikiana na wananchi wa Tanzania zaidi ya mikutano inayofanyika nda ili wajionee ukarimu wa Watanzania, utajiri wa utamaduni wetu, na uzuri wa nchi yetu.
Kuanzia katika tambarare zisizo na mwisho za Serengeti, Mlima Kilimanjaro unaosimama kwa fahari, hadi visiwa vya kuvutia vya Zanzibar vyenye mandhari ya kipekee,
Ambapo Tanzania inatoa uzoefu wa kukumbukwa pamoja na fursa nyingi katika sekta za utalii, ukarimu, na maendeleo endelevu.
Chukueni muda wa kuvitembelea na kuvifurahia. Mko tayari hapa; tumieni fursa hii vizuri kabla ya kurejea makwao ili msilazimike kununua tiketi nyingine ili warudi tena.
Napenda pia kushiriki nanyi fahari yetu ya kuwa wenyeji, kwa kushirikiana na nchi jirani za Kenya na Uganda, wa michuano ya kihistoria ya Kombe la Mataifa ya Afrika (TotalEnergies CAF Africa Cup of Nations – AFCON PAMOJA 2027).
Hii itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa michuano ya AFCON kufanyika Afrika Mashariki, na pia mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu.
Hatua hii ni ushahidi si tu wa mapenzi yetu ya pamoja kwa michezo, bali pia wa kuongezeka kwa imani ya Afrika katika uwezo wake wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa kwa viwango vya hali ya juu, huku ikiimarisha ushirikiano wa kikanda na uwekezaji katika sekta ya michezo.
Kama Waafrika, tunapofanya kazi kwa pamoja, hakuna kikomo cha kile tunachoweza kukifikia.
Xxx


