Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
Zaidi ya wananchi 420 wamepata ajira zisizo za ujuzi kupitia utekelezaji wa ujenzi wa Kituo cha Kuongeza Msukumo wa Mafuta (PS4) cha Mbogwe, kinachotekelezwa chini ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Hayo yameelezwa Agosti 8, 2026 na Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Derick Moshi, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kilichopo Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita.
Bw. Moshi amesema utekelezaji wa mradi huo umeendelea kutoa manufaa kwa Watanzania, ambapo takribani asilimia 80 ya fursa zinazotokana na mradi zimenufaisha Watanzania, ikiwemo ajira, mafunzo na ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.
Amesema zaidi ya ajira hizo, mradi umetoa mafunzo kwa wananchi kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), hatua iliyowawezesha kupata ujuzi na uzoefu unaohitajika katika kushiriki kwenye miradi mikubwa ya kimkakati.
“Mradi huu umeendelea kuwa fursa kwa Watanzania, siyo tu kupitia ajira, bali pia kupitia mafunzo yanayowawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema Bw. Moshi.
Aidha, Bw. Moshi ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa PS4, ambao umefikia asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.
Amesema utekelezaji wa mradi huo umezingatia pia ushirikishwaji wa jamii inayozunguka mradi kupitia ajira, utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) pamoja na maboresho ya miundombinu, ikiwemo barabara na huduma za maji.
Ameeleza kuwa vituo vya kuongeza msukumo wa mafuta vya Muleba (PS3) na Mbogwe (PS4) ni sehemu muhimu ya miundombinu ya EACOP, kwa kuwa vina jukumu la kupokea na kuongeza msukumo wa mafuta ili yaweze kusafirishwa kwa ufanisi kupitia bomba hilo kuelekea kituo cha mwisho cha Kiteto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Huduma wa EACOP ambaye pia ni Kaimu Meneja wa EACOP Tanzania, Bw. Geofrey Mponda, amesema vituo vya kuongeza msukumo wa mafuta ni miundombinu muhimu katika kuhakikisha usafirishaji wa mafuta kupitia EACOP unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Amesema utekelezaji wa Mradi wa EACOP umeendelea kuwa chachu ya fursa kwa Watanzania, hususan vijana, kwa kuwa umetoa ajira kwa wenye ujuzi na wasio na ujuzi, huku ukiwawezesha pia kupata uzoefu wa vitendo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
“EACOP imeendelea kuwa chachu ya fursa kwa Watanzania. Vijana wamepata ajira na wengine wamepata fursa ya kujifunza na kujenga uzoefu ambao utawasaidia kushiriki katika miradi mingine mikubwa ya kimkakati,” amesema Mponda.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya EACOP katika eneo la mradi (EACOP Company Site Representative), Bw. Kamal Maalouli, amesema PS4 ni miongoni mwa vituo vikubwa na muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa EACOP.
Amesema kampuni imeendelea kuweka juhudi zote kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika kwa wakati uliopangwa na kukidhi viwango vinavyohitajika ili kiweze kutekeleza jukumu lake katika mfumo wa usafirishaji wa mafuta kupitia EACOP.
Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania, ambapo sehemu kubwa ya bomba hilo inapita nchini Tanzania.











