Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umeendelea kuimarisha usajili wa matukio muhimu ya binadamu nchini kwa kutumia mifumo ya kidijitali na kusogeza huduma karibu na wananchi, hatua inayolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata nyaraka muhimu za utambulisho na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na Serikali kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali ya RITA, kuongeza uhamasishaji kwa wananchi na kuboresha upatikanaji wa huduma za usajili wa matukio muhimu ya binadamu, ikiwemo vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto wa kuasili.
Dkt. Homera aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika (CRVS Day 2026), yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma hizo zinamfikia kila mwananchi bila kujali mahali anapoishi au hali yake ya kiuchumi, huku ikiendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili matukio muhimu yanayotokea katika maisha ya binadamu, akisisitiza kuwa usajili huo pia una nafasi kubwa katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa.
“Siku hii ni fursa ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili matukio kama vile vizazi, vifo, ndoa, talaka na matukio mengine muhimu yanayotokea katika maisha ya binadamu,” amesema Dkt. Homera.
Alisisitiza kuwa usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni urithi wa kitaifa na alama ya heshima kwa kila mwananchi, huku ukitoa msingi muhimu wa upatikanaji wa takwimu zinazotumika katika kupanga na kusimamia maendeleo ya taifa.
“Maendeleo ya Taifa hayawezi kutenganishwa na upatikanaji wa takwimu sahihi na zinazotegemeka,” alieleza Dkt. Homera.
Kwa mujibu wa Dkt. Homera, takwimu za RITA zinaonyesha kuwa usajili wa vizazi kwa watoto umeendelea kuongezeka, kutoka asilimia 55 mwaka 2020 hadi asilimia 68 mwaka 2025, huku Serikali ikiwa na lengo la kufikisha kiwango hicho hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Aliipongeza RITA kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kusimamia na kuratibu usajili wa matukio muhimu ya binadamu, akisema huduma hiyo inasaidia kujenga mifumo ya Serikali yenye taarifa sahihi, salama na zinazoweza kutumika kwa wakati zinapohitajika.
“Nipende kuwapongeza RITA kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuhakikisha wanasimamia na kuratibu usajili wa matukio muhimu ya binadamu na hivyo kuwezesha kujenga mifumo ya Serikali yenye taarifa sahihi, salama na zinazoweza kutumika wakati zinapohitajika,” amesema.
Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza mwamko na kasi ya wananchi kusajili matukio muhimu ya binadamu mara tu yanapotokea.
Amesema RITA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kusogeza huduma hizo kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za usajili na utoaji wa vyeti kwa makundi yenye mahitaji maalum.
“Katika kuadhimisha siku hii, Wakala umefanikisha kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 161 wenye mahitaji maalum kutoka Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo mkoani Dodoma, pamoja na watoto 320 kutoka Kata ya Mtwango wilayani Mufindi, mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya kujali na kurejesha kwa jamii, hasa makundi yenye mahitaji maalum,” amesema Kanyusi.
Kanyusi pia amesema mwitikio wa wananchi katika huduma za usajili umeongezeka tangu kuzinduliwa kwa mpango wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vifo ndani ya saa 48 za kazi, uliozinduliwa Desemba 12, 2025.
Amesema tangu kuzinduliwa kwa mpango huo hadi Agosti 9, 2026, RITA imepokea jumla ya maombi 776,698, ambapo maombi 756,570 yalihusu usajili wa vizazi na 20,127 yalihusu usajili wa vifo.
“Jumla ya maombi 755,973 yalikidhi vigezo na vyeti kutolewa ndani ya saa 48 za kazi, sawa na asilimia 97.3 ya maombi yaliyokidhi vigezo,” alisema Kanyusi.
Alifafanua kuwa kati ya maombi yaliyokidhi vigezo, maombi 737,416 yalikuwa ya vizazi, huku 18,556 yakiwa ya vifo.
Aidha, Kanyusi alisema jumla ya maombi 20,725 hayakukidhi vigezo na hivyo kurejeshwa kwa waombaji kwa ajili ya kufanya marekebisho na kuwasilisha viambata vinavyothibitisha kutokea kwa matukio husika.
Alisema kati ya maombi hayo, 19,154 yalihusu usajili wa vizazi, huku 1,571 yakiwa ya vifo.
Kwa upande wake, Meneja wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, Bw. Darius Kalijongo, ameishukuru Serikali kupitia RITA kwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata vyeti vya kuzaliwa, akisema nyaraka hizo zinawapa watoto hao haki yao ya msingi ya kutambulika na kupata huduma mbalimbali.
Kalijongo alisema vyeti vya kuzaliwa vitawasaidia watoto hao kupata huduma muhimu zikiwemo mahitaji ya shule, huduma za afya, ajira, makazi na huduma nyingine za kijamii.
“Tunaiishukuru RITA kwa namna inavyojali na kuthamini haki ya msingi na hivyo kurejesha kwa jamii, hususani makundi yenye mahitaji maalum. Kwa kufanya hivyo, itawasaidia watoto hawa 161 kupata nyaraka nyingine muhimu za utambulisho, ikiwemo Kitambulisho cha Taifa (NIDA), kupata mikopo ya elimu ya juu, fursa za kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika masuala yote ya kijamii na kitaifa,” alisema Kalijongo.
Amesema upatikanaji wa vyeti hivyo ni hatua muhimu katika kuwawezesha watoto hao kukua wakiwa na utambulisho rasmi na kupata fursa sawa na wananchi wengine katika kupata huduma na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu (2026–2036): Kuimarisha Mafanikio ya Mpango wa Afrika wa Kuharakisha Uboreshaji wa Usajili na Takwimu za Matukio Muhimu kwa Mustakabali Endelevu kupitia Utengamano, Ugatuzi na Teknolojia za Kidijitali.”
Kaulimbiu hiyo inaweka msisitizo katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, ugatuzi wa huduma na utengamano wa mifumo ya usajili na takwimu ili kuongeza upatikanaji wa huduma, kuboresha ubora wa taarifa na kuwezesha Serikali kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kutumia takwimu sahihi na zinazotegemeka.







