Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema juhudi za usambazaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia zinapaswa kwenda sambamba na kuweka mkazo katika mabadiliko ya mila, desturi na mitazamo ambayo inachangia katika kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo Agosti 11, 2026, Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar wakati wa Mdahalo wa Nishati Safi ulioandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), uliowakutanisha Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha, wanateknolojia, watafiti na asasi za kiraia uliolenga kujadili namna ya kuongeza kasi ya upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyo endelevu na nafuu kwa wananchi na taasisi.
“Licha ya kuwa na mkakati wa nishati safi ya kupikia, tusipowekeza katika kubadili mila na desturi zetu tutajikuta pale pale. Wakati tunasukuma matumizi ya teknolojia, tuwekeze pia katika kubadili mitazamo ya Watanzania kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Mhe. Ndejembi.
Ameongeza kuwa mabadiliko hayo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi na jamii yenyewe ili kuondoa mitazamo na desturi zinazoweza kuwa kikwazo katika kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, Mhe. Ndejembi
amewasisitiza watendaji wa Wizara, Taasisi na sekta binafsi kulipa umuhimu suala la kuweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia mchanganyiko za nishati safi ya kupikia kulingana na rasilimali zinazopatikana katika maeneo husika mfano ni maeneo yenye upatikanaji wa samadi ambayo inaweza kutumika kuzalisha bayogesi ili kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Ndejembi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji anaoufanya katika nishati safi ya kupikia ambapo ameiweka Tanzania katika nafasi ya kuonesha kuwa nishati safi ya kupikia si suala la matumizi ya kaya pekee, bali inagusa afya, mazingira, uchumi, usawa wa kijinsia, elimu na maendeleo endelevu.
Amesema tangu kuzinduliwa kwa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali imeongeza uelewa wa wananchi kupitia kampeni na maonesho ya nishati safi, sambamba na kuanzisha na kupanua miradi mbalimbali, ikiwemo utoaji wa ruzuku ya mitungi na majiko kwa kaya zilizopo vijijini na pembezoni mwa miji.
Hatua nyingine ni kuanzishwa kwa miradi ya kulipia majiko ya umeme kupitia bili za umeme (on-bill financing), ufungwaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, pamoja na kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika gesi, mitungi, matanki, mita janja za LPG na mashine za kutengeneza mkaa mbadala.
Amesema Serikali pia imeimarisha uratibu baina ya wizara na taasisi za Serikali, huku ushiriki wa sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo ukiendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, mafanikio hayo yamechangia kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo yanayopewa msisitizo na Serikali ni kuwezesha taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, zikiwemo shule, hospitali, magereza, vyuo na vituo vya mafunzo, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa kwa sasa ni taasisi 2,616 pekee kati ya taasisi 31,395 zinazotumia nishati safi ya kupikia hali inayoonesha ukubwa wa kazi iliyopo mbele katika kufikia malengo yaliyowekwa.
Kutokana na ukubwa wa mahitaji hayo, Mhe. Ndejembi amesema mabadiliko hayawezi kufanikishwa kwa kutegemea bajeti ya Serikali pekee, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na uhamasishaji wa rasilimali fedha (partnerships and resource mobilization).
Hivyo, ametoa wito kwa taasisi za fedha kubuni mikopo nafuu itakayowezesha shule, hospitali na taasisi nyingine kuwekeza katika nishati safi bila kulazimika kulipa gharama zote za awali kwa wakati mmoja.
Pia ameihimiza sekta binafsi kuja na mifumo bunifu ya kifedha, ikiwemo malipo kwa awamu na mikopo yenye masharti nafuu.
Vilevile, ametoa wito kwa washirika wa maendeleo kushirikiana na Serikali kufadhili miradi inayoweza kuzifikia taasisi nyingi zaidi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamisha miradi kutoka hatua za majaribio (pilots) kwenda kwenye uwekezaji wa kiwango kikubwa na wa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Mhe.Ndejembi ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea na maandalizi ya Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Zanzibar akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama, nafuu na endelevu ya kupikia.
Amesema Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kufikia malengo hayo, ikiwemo kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa mkakati, mifumo ya uratibu, uhamasishaji wa rasilimali, ushirikishwaji wa sekta binafsi, ukusanyaji wa takwimu na ufuatiliaji wa utekelezaji..
Vilevile ameipongeza MIF kwa kuifanya nishati safi ya kupikia kuwa miongoni mwa ajenda zake muhimu na kwa kuandaa mdahalo wenye mafanikio uliowakutanisha wadau muhimu wa nishati safi ya kupikia.










