Na. Asia Singano, WF – Dodoma

Wizara ya Fedha imeendesha mafunzo kwa wajumbe na wenyeviti wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya usimamizi, ushauri na ufuatiliaji wa utendaji wa Idara/vitengo vya ukaguzi wa ndani na mifumo ya udhibiti wa ndani katika taasisi za Serikali.

Akizungumza wakati wa kufungua Mafunzo hayo, Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wajumbe kuelewa kwa kina wajibu wao katika kuhakikisha shughuli za ukaguzi wa ndani zinafanyika kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia misingi ya maadili ya taaluma.

Alitoa rai kwa kamati hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, weledi, uhuru na uwajibikaji ili kuimarisha mfumo wa usimamizi wa rasilimali na udhibiti wa ndani Serikalini.

‘’Nawahimiza kutekeleza majukumu yenu inavyopaswa kwa kuzingatia nidhamu pia kuhakikisha vikao vinafanyika kwa mujibu wa ratiba, wajumbe wanapata taarifa muhimu kwa wakati na wanajiandaa kabla ya vikao” Alisema Mhandisi Nindie.

Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kuongeza weledi na kutumia teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya katika kazi za ukaguzi, kwa kuwa matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa hatua muhimu za kuboresha utendaji wa shughuli za ukaguzi.

Alisema mabadiliko ya teknolojia yanaendelea kuathiri namna kazi za ukaguzi zinavyotekelezwa, hivyo ni muhimu kwa wakaguzi kuendana na mabadiliko hayo na kuhakikisha wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya kazi.

Awali, akimkaribisha Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Paison Mwamnyasi, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyazingatia kwa umakini ili kufikia lengo lililokusudiwa la mafunzo hayo.

‘’Mafunzo haya yana umuhimu sana kwenye utendaji wetu hivyo ni muhimu kuyazingatia ili kuleta matokeo chanya yaliyolengwa na Wizara’’ alisema Bw. Mwamnyasi.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkaguzi wa Ndani Mwandamizi kutoka Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Andrew Nicholaus, alieleza kuwa Kamati ya Ukaguzi ina jukumu muhimu la kusaidia mamlaka inayoteua katika kutekeleza wajibu wake wa usimamizi, huku ikitakiwa kubaki huru katika kutoa ushauri na uangalizi.

Mafunzo hayo yanayoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Wizara ya Fedha, ya kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani na Kamati za Ukaguzi wa ndani kama sehemu ya juhudi za kuongeza uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali.