Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

JUMLA ya silaha za moto 17 na risasi 19 zimesalimishwa kwa hiari katika Vituo vya Polisi na Ofisi za Serikali za Vijiji na Kata Mkoani Tabora kufuatia zoezi linaloendelea nchi nzima la usalimishaji silaha haramu kwa hiari bila kushtakiwa.

Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Twaha Lulengelule alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ambapo ameeleza kuwa zoezi hilo limeanza Septemba 1, 2026 na litamalizika Oktoba 31, 2026.

Alifafanua kuwa zoezi hilo linaloendeshwa na Jeshi la Polisi nchi nzima limelenga kuhakikisha silaha haramu zote zikiwemo zile zinazomilikiwa na watu au taasisi kinyume na taratibu zinasalimishwa kwa hiari kwa msamaha pasipo kushtakiwa.

‘Zoezi hili ni muhimu sana, naendelea kutoa wito kwa wananchi kutekeleza kwa hiari kabla ya kipindi cha msamaha wa kutokushtakiwa kumalizika ifikapo Oktoba 31, 2026 kinyume na hapo mkondo wa sheria utachukua nafasi yake’, alieleza.

Kamanda Lulengelule alipongeza wananchi wanaotoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao kwa Jeshi hilo na kuwataka kuendelea kufanya hivyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka dhidi ya wahusika wote.

Alibainisha kuwa kati ya silaha zilizosalimishwa, 9 ni aina ya short gun na risasi 15 za rifle ambazo zilisalimishwa katika Vituo vya Polisi na Kampuni binafsi za ulinzi katika Wilaya ya Nzega na Tabora Mjini kwa kukosa sifa za umiliki halali.

Na zingine 8 zikiwemo Gobole zilizotengenezwa kienyeji na risasi 4 zilisalimishwa na wananchi katika Ofisi za Serikali ya Kijiji na Kata katika Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa.