Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray ametimiza ahadi yake ya kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mwinkansi Kata ya Mamire.

Naibu Waziri Ndege amekabidhi mifuko hiyo 100 ya saruji ili kutimiza ahadi hiyo aliyoitoa wakati wa sherehe za Jubilee ya kwaya ya Parokia ya Mamire.

Wananchi wa eneo hilo na Diwani wa Kata ya Mamire walimuomba msaada wa daraja hilo muhimu kwa wanafunzi na wakazi hao kupata huduma upande wa pili.

Naibu Waziri Ndege ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara’, aliambatana na Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa huo, Fatuma Tsea, viongozi wa CCM, Serikali pamoja na wananchi walijitokeza kwa wingi katika makabidhiano hayo.

Baadhi ya wakazi wa Mwinkansi wamemshukuru Naibu Waziri Ndege kwa kuwapatia mifuko 100 ya saruji ili iweze kutumika kujengea eneo hilo.

Wakazi hao wameeleza kwamba kutokana na umuhimu wa daraja hilo, walishaanza kuchangishana wenyewe kwa wenyewe ili kulijenga kabla ya msaada huo.

Wakazi hao na wanafunzi wamemshukuru Naibu Waziri Ndege kwa hatua hiyo ya kuwaunga mkono.

Akizungumza nao Naibu Waziri Ndege ameahidi kuendelea kulisemea daraja hilo katika ngazi za juu ili kurejesha mawasiliano ya jamii hasa wakati wa mvua ambapo daraja hilo lilikatika.

Daraja la Mwinkansi ni kiungo muhimu kwa wanafunzi kwenda shule na wananchi kwenda kupata huduma za afya, mahitaji ya masoko na matumizi mengine.