Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa Wizara ya Afya kuacha kujifungia ofisini kwa kuwa uongozi bora unahitaji ushirikiano, mawasiliano ya wazi na kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo ya taasisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Mafunzo ya Tafakuri (Retreat) ya viongozi na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Afya ambapo amesisitiza umuhimu wa viongozi kuelewa athari za maamuzi yao kwa watumishi, utendaji wa taasisi na utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
“Kila kiongozi anapaswa kutambua kuwa taasisi ina dira, malengo na majukumu ya pamoja, hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi hiyo badala ya kutanguliza maslahi binafsi, ushindani usio na tija au tofauti zinazoweza kudhoofisha mshikamano katika utekelezaji wa majukumu,” amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kujenga mazingira ya kazi yanayowezesha watumishi kushirikiana, kushauriana na kutatua changamoto kwa pamoja, akieleza kuwa mafanikio ya taasisi yanategemea namna watu wanavyounganisha ujuzi, uzoefu na uwezo wao katika kufikia malengo yaliyowekwa.
Dkt. Magembe amegusia pia umuhimu wa kuzingatia uwajibikaji na haki katika usimamizi wa watumishi, akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuheshimiwa kulingana na mchango wake.
“Vilevile, ni muhimu kuhakikisha mifumo ya kazi inawezesha wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku changamoto za kiutendaji zikishughulikiwa kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,” amesema Dkt. Magembe
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa viongozi kufuatilia utekelezaji wa majukumu na kutathmini matokeo ya maamuzi wanayoyafanya, badala ya kuishia kutoa maelekezo bila kujua kama yameleta mabadiliko yaliyokusudiwa.
Mafunzo hayo ya Tafakuri yanatoa fursa kwa viongozi na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Afya kutathmini utendaji wa kazi, kujadili changamoto zinazokabili utekelezaji wa majukumu na kuweka mikakati ya kuimarisha usimamizi, ushirikiano na ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini.












