
KATIKA mazingira ya sasa, ambapo bei za bidhaa za mafuta katika soko la dunia zinabadilika kutokana na migogoro ya kimataifa, gharama za usafirishaji na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha, usimamizi wa bei una umuhimu mkubwa katika kulinda maslahi ya wananchi na uchumi wa taifa.
Nchini Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ina jukumu la kusimamia bei katika sekta inazozidhibiti kwa mujibu wa sheria. Katika sekta ndogo ya mafuta, EWURA hutangaza bei kikomo za petroli, dizeli na mafuta ya taa ili kuhakikisha kuwa bei zinazotozwa zinazingatia gharama halisi na utaratibu wa udhibiti uliowekwa.
Kwa nini EWURA inatangaza bei?
Lengo la EWURA si kufanya mafuta yawe na bei ya juu, bali kuhakikisha kuwa bei zinazotozwa ni za haki, zinazingatia mwenendo wa soko na kulinda maslahi ya watumiaji pamoja na watoa huduma.
Katika kupanga bei kikomo za mafuta, EWURA huzingatia gharama mbalimbali, zikiwemo bei za ununuzi katika soko la dunia, usafirishaji, bima, viwango vya ubadilishaji fedha, kodi, tozo na gharama nyingine zinazotambuliwa katika mfumo wa ukokotoaji wa bei.
Mwananchi anafaidikaje?
Kwanza, bei kikomo humlinda mwananchi dhidi ya kutozwa bei zinazozidi kiwango kilichoidhinishwa. Hii husaidia kuzuia baadhi ya wafanyabiashara kutumia mabadiliko ya soko kuongeza bei kiholela.
Pili, utangazaji wa bei huongeza uwazi. Mwananchi anaweza kujua bei inayopaswa kutozwa katika eneo lake na hivyo kuwa na msingi wa kudai haki yake anaponunua mafuta.
Tatu, usimamizi wa bei husaidia kuweka uwiano kati ya maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara, ili wananchi wapate bidhaa kwa bei zinazozingatia gharama huku biashara zikiendelea kuwa endelevu.
Uchumi wa taifa unanufaikaje?
Mafuta ni bidhaa muhimu katika shughuli za uchumi. Hutumika katika usafirishaji wa abiria na mizigo, kilimo, viwanda na utoaji wa huduma mbalimbali.
Kwa hiyo, usimamizi wa bei unaozingatia gharama na uwazi husaidia biashara kupanga matumizi, kupunguza uwezekano wa utozaji wa bei holela na kuongeza utabirika wa gharama katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, mfumo wa bei unaotabirika na unaozingatia gharama unaweza kusaidia kudumisha ushindani wa haki, kulinda uwekezaji na kuwezesha upatikanaji endelevu wa bidhaa za mafuta nchini.
Nini kinaweza kutokea EWURA isipotangaza bei kikomo?
Katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya bei za mafuta duniani, kutokuwepo kwa bei kikomo na mfumo madhubuti wa usimamizi kunaweza kuongeza hatari ya baadhi ya wafanyabiashara kutoza bei kubwa zisizoendana na gharama halisi.
Hali hiyo inaweza kuongeza gharama za usafirishaji, uzalishaji na maisha ya wananchi. Pia, inaweza kupunguza uwazi wa bei na kufanya iwe vigumu kwa watumiaji kutambua iwapo wanatozwa bei inayostahili.


