Na Deodatus Balile,JamhuriMedia, Bukoba
Kitambo sasa nimefuatilia juhudi za Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, kutatua migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi. Kila anapoingilia mgogoro, tunashuhudia akitoa maelekezo, watendaji wakiwajibishwa na wananchi wakipata matumaini. Lakini najiuliza, kwa nini migogoro hii inasubiri Waziri Mkuu?
Nimetafakari kwa kina na kufikia hitimisho kwamba sehemu kubwa ya migogoro nchini inachochewa na watumishi wa umma kutotekeleza wajibu wao ipasavyo. Wapo wanaolipwa mishahara kwa kazi ambazo hawazifanyi kwa kiwango kinachostahili.
Sitanii, tembelea baadhi ya ofisi za umma. Utakuta watumishi wamejikusanya kwenye makundi ya WhatsApp, wakijadili siasa, mpira, majungu na maisha ya watu. Saa za kazi zinapotea huku wananchi wakisubiri huduma. Mshahara unapoingia mwisho wa mwezi, kila mmoja anataka alipwe kikamilifu!
Ugonjwa huu haupo serikalini pekee. Hata sekta binafsi upo. Tofauti ni kwamba sekta binafsi ina mifumo inayowezesha kuchukua hatua za kinidhamu kwa haraka zaidi, ingawa haki za wafanyakazi lazima zilindwe.
Tumefikia mahali baadhi ya watu wanakubali mishahara midogo ili mradi wapate uhakika wa ajira, yaani job security. Kwao, uhakika huo umegeuka kinga ya kutowajibika badala ya kuwa motisha ya kufanya kazi. Wapo waliotumia uhakika huo kuwa na kiburi cha kufa mtu.
Nitakupeni mfano. Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu, mara kadhaa ameagiza askari wa usalama barabarani wasikamate magari na pikipiki na kuzipeleka vituoni. Kinachotokea ni kichekesho. Polisi wanasema bila aibu kuwa hayo ni maelekezo ya kisiasa. Maisha yanaendelea kama kawaida.
Sitanii, ipo sababu. Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, pamoja na kanuni zake, inahitaji kuangaliwa upya. Fikiria dereva akimpiga kibao waziri! Waziri huyo hawezi kumfukuza papo hapo bila kufuata taratibu za kinidhamu. Sipingani na haki ya mtumishi kusikilizwa. Ninachopinga ni taratibu zinazoweza kufanya uwajibishaji uchelewe au kuondoka kwa kiasi cha kuathiri huduma kwa wananchi.
Angalia hospitali zetu. Mganga Mkuu anaweza kuwa na jukumu la kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa, lakini mamlaka yake ya kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya watumishi yanaweza kuwa na mipaka. Daktari au nesi anaposhindwa kutekeleza wajibu wake, mgonjwa ndiye anayeteseka, ila Mganga Mkuu hana cha kumfanya.
Hali hii inajitokeza pia kwenye ardhi. Mwananchi mmoja anapewa kiwanja, mwingine anapewa hati kwenye eneo hilohilo. Migogoro inaanza, familia zinagombana, fedha zinatumika mahakamani na wakati mwingine damu inamwagika. Wanaosababisha migogoro hiyo wanaweza kuendelea na kazi kwa miaka mingi wakati wananchi wakiteseka. Je, tunahitaji Waziri Mkuu afuatilie kila hati ya ardhi nchini?
Sitanii, tusimgeuze Mwigulu kuwa zimamoto wa makosa yanayozalishwa na watendaji wasiotimiza wajibu wao. Tunachohitaji ni mageuzi ya sheria, kanuni na mifumo ya uwajibikaji. Wakuu wa taasisi wapewe mamlaka yanayoendana na majukumu yao, ikiwamo kuajiri na kufukuza kazi, japo uamuzi wao udhibitiwe kuzuia uonevu na upendeleo.
Mtumishi anayefanya kazi vizuri alindwe na athaminiwe. Anayezembea awajibishwe kwa wakati. Anayefanya makosa makubwa achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria haraka. Ninampongeza Dk. Mwigulu kwa juhudi zake, lakini mafanikio yake yawe kichocheo cha mabadiliko ya kudumu.
Sitanii, tusijenge taifa ambalo kila tatizo linahitaji Waziri Mkuu. Tujenge taifa ambalo kila mtumishi anatimiza wajibu wake! Kimsingi, anaposikiliza migogoro, huwa najiuliza: Katika wilaya au mikoa hii kuna viongozi kweli? Inaumiza mno. Tubadili sheria, unyampara uje, vinginevyo tutabadilishwa sisi. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827

