Na Mwandishi Wetu, JamahuriMedia, Musoma
Utata umegubika kifo cha mkazi wa Butiama, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Josephat Warioba, baada ya ripoti ya uchunguzi wa mwili (postmortem) kubaini kuwa alipigwa kichwani na kitu butu, hali inayokinzana moja kwa moja na maelezo ya awali ya Jeshi la Polisi yaliyodai aligongwa na bodaboda.
Tangu alipopigwa Agosti, mwaka huu, polisi wamekwama kuwakamata watuhumiwa licha ya kuwa wanafahamika.
Warioba, aliyekuwa akiishi kwa kutegemea kazi za vibarua wilayani Butiama, alifariki dunia mchana wa Septemba 5, mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki tatu akiwa katika hali ya kutojitambua.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu na watoa taarifa wa karibu wa familia hiyo, alishambuliwa na kupigwa mara mbili tofauti – Julai 28 na Agosti 2, mwaka huu na watu wanaofahamika. Tukio kwanza lilitokea katika Kijiji cha Bumangi, na la pili Butiama.
Hata hivyo, licha ya majina ya wahusika kufahamika na ndugu wa marehemu kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wilayani Butiama, hadi mwili wa Warioba unazikwa nyumbani kwao Butiama Septemba 11, hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa.
Mabadiliko ya lugha kutoka kwa Polisi Mkoa wa Mara kudai kuwa marehemu alipata ajali ya kugongwa na bodaboda yamepingwa vikali na familia na wadau waliofuatilia tukio hilo, wakisisitiza kuwa wana ushahidi wa kutosha wa namna alivyoshambuliwa.
Msimamo huo wa familia umepata nguvu zaidi kutokana na majibu ya upasuaji wa uchunguzi wa mwili uliofanyika Septemba 8, mwaka huu; siku tatu baada ya kifo chake – ambako ripoti ya daktari ilithibitisha kuwa chanzo cha majeraha makubwa yaliyosababisha mauti yake ni kupigwa sehemu za kichwani kwa kutumia kitu butu. “Naziomba mamlaka zimtendee haki maskini huyu kwa kuwawajibisha wote walioshiriki kumpiga na kumfanya awe kwenye koma kwa muda wote huu na hatimaye ameaga dunia.
KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 17 – 23, 2026

