WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Majeshi ya Polisi yaliyo katika nchi za Kusini mwa Afrika chini ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi (SARPCCO) kutumia teknolojia za kisasa na kubadilishana taarifa za kiintelijensia ili kudhibiti mitandao ya uhalifu unaovuka mipaka.
Wito huo ameutoa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 30 wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi wanachama wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa Kusini mwa Afrika (SARPCCO) uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Bashungwa amesema changamoto kama ugaidi, wizi wa magari, biashara haramu ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu na uhalifu wa mtandao zinahitaji ushirikiano wa karibu na mikakati ya pamoja inayotumia teknolojia za kisasa.
“Lazima tushirikiane kwa karibu zaidi, tuwekeze kwenye mifumo ya kidijitali ya kiintelijensia, na tuimarishe mafunzo ya pamoja ili kuhimili kasi ya wahalifu wanaozidi kutumia mbinu za kisasa”, amesema.

Katika mkutano huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura, alikabidhi rasmi uenyekiti wa SARPCCO kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa nchi ya Malawi Merlyne Yolamu.
IGP Wambura alipongeza uteuzi huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na uongozi mpya huku akielezea mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wake ikiwemo kuimarika kwa uratibu wa oparesheni za pamoja na mafunzo ya kiufundi kwa maafisa wa polisi wa nchi wanachama.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Malawi Merlyne Yolamu amesema kuwa uteuzi wake ni heshima kubwa na anauchukulia kama wajibu wa kipekee.
Aliahidi kuwa chini ya uongozi wake shirikisho hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu ili kushughulikia changamoto za uhalifu wa mipakani, hasa ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, na uhalifu wa kidijitali.
“Tutahakikisha SARPCCO inakuwa chombo madhubuti cha ushirikiano wa kiusalama kwa nchi zetu”, amesema

.SARPCCO ni jukwaa la ushirikiano wa nchi 16 za Kusini mwa Afrika, Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesotho, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Eswatini, Madagascar na Shelisheli.
Mkutano huu wa 30 unalenga kuimarisha mshikamano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka na kuendeleza amani, usalama na utulivu katika kanda.
