Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amepokea msaada wa ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 kutoka Taasisi ya Kimataifa ya IDDef ya nchini Uturuki, kwa ajili ya kuwawezesha waumini wa Kiislamu kushiriki ibada ya kuchinja katika Sikukuu ya Eid Al-Adha.

Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Taasisi ya IDDef, Abdul Hamid Khann, amesema ,sadaka hiyo imelenga kusaidia Waislamu katika Mkoa wa Pwani kutekeleza ibada muhimu ya kuchinja, kama sehemu ya utamaduni na imani ya Kiislamu ulimwenguni kote wakati wa Idd.

Nae Kunenge ameishukuru taasisi hiyo kwa mchango huo na kuwahakikishia waumini kuwa mifugo yote iliyotolewa ni mizima na inafaa kwa matumizi ya kitoweo.

Aidha, amebainisha Serikali ya Mkoa imeandaa utaratibu maalum wa kuhakikisha msaada huo unagawiwa kwa haki na usawa kwa waumini katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Kwa niaba ya Sheikh wa Mkoa, Kadhi wa Mkoa wa Pwani, Sheikh Rashid Changunda , amesema msaada huo ni wa baraka na ni ishara ya mshikamano wa kidini na kibinadamu.