Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetangaza kuwachagua wanafunzi 214,141 wenye sifa za kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka wa masomo 2025.

Idadi hiyo inajumuisha wanafunzi 1,028 wenye mahitaji maalumu na kwamba uchaguzi huo umezingatia vigezo vya ufaulu, sera ya elimu, mtaala mpya ulioboreshwa na kuimarika kwa miundombinu ya elimu nchini.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema ongezeko la idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kutoka 188,787 mwaka 2024 hadi 214,141 mwaka huu linatokana na kuongezeka kwa ufaulu na juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, kati ya wanafunzi hao, 149,818 sawa na asilimia 69.96 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule 694 za serikali. Kati yao, wasichana ni 76,491 na wavulana 73,327.

Alisema hilo ni ongezeko kutoka wanafunzi 131,986 waliochaguliwa mwaka 2024. Kati yao, wanafunzi 1,728 (wasichana 801 na wavulana 927) wamepangwa katika shule nane maalumu za vipaji zenye kupokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi.

Alisema wanafunzi 141,146 wamepangiwa shule za bweni wakiwamo wasichana 72,337 na wavulana 68,809, huku wanafunzi 6,944 (wasichana 3,353 na wavulana 3,591) wakipangwa katika shule za kutwa.

Kwa upande wa elimu ya ufundi, alisema wanafunzi 2,875 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi vya Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI). Kati yao, wasichana ni 1,057 na wavulana 1,818. Aidha,

Mchengerwa alisema wanafunzi 2,214 (wasichana 1,099 na wavulana 1,115) wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya stashahada, na 1,609 (wasichana 443 na wavulana 1,166) wamepangiwa kujiunga na vyuo vya ualimu kwa ngazi hiyo.

“Wanafunzi wengine 57,625 (wasichana 18,427 na wavulana 39,198) wamepangiwa vyuo vya kada mbalimbali nchini,” alisema Mchengerwa.

Alisema wanafunzi wa Kidato cha Tano wanapaswa kuripoti shuleni kuanzia Julai 6 hadi Julai 21, 2025, huku muhula wa kwanza ukitarajiwa kuanza rasmi Julai 8, 2025.

Kwa upande wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi, alisema kila mwanafunzi atapokea maelekezo ya taratibu za kujiunga kupitia chuo alichopangiwa.

Alisisitiza kuwa mchakato wa uchaguzi umezingatia vigezo vya ufaulu na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko ya shule.