Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imeendelea kusikiliza shauri la jamii ya Ogiek kutoka Kenya dhidi ya serikali ya nchi hiyo, wakidai kutotekelezwa kwa maamuzi ya awali ya Mahakama kuhusu haki zao za ardhi, fidia na utambuzi rasmi wa jamii hiyo.

Kesi hiyo ilihusiana na kutotekelezwa kwa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hiyo Mei 26, 2017, na maamuzi ya utekelezaji ya Juni 23, 2022, ambayo yaliitaka Kenya kutoa fidia na kurejesha jamii ya Ogiek katika ardhi yao ya asili iliyoko katika Msitu wa Mau.

Katika kikao hicho mvutano wa kisheria uliibuka kati ya mawakili wa serikali ya Kenya na wale wa upande wa jamii ya Ogiek wakiongozwa na Profesa wa Sheria Dr. Solomon Dersso kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini.

Nje ya Mahakama, kiongozi wa jopo la mawakili upande wa Ogiek wakili Bahame Nyanduga alieleza waandishi wa habari kuwa licha ya ushindi katika kesi hiyo lakini serikali ya Kenya haijatekeleza maamuzi ya Mahakama kwa zaidi ya miaka saba tangu uamuzi wa awali na miaka mitatu tangu uamuzi wa pili wa utekelezaji.

Mahakama ilitaka kujua kama Jamhuri ya Kenya imetekeleza maagizo yote mawili ambapo serikali ilijibu kuwa utekelezaji wake umeathiriwa na changamoto za kifedha na hitaji la ushirikiano kutoka taasisi mbalimbali ingawa ilikiri kutambua haki ya jamii ya Ogiek.

Serikali ya Kenya pia ilieleza kuwa iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na ikaomba Mahakama iwaongezee muda jambo lililopingwa vikali na upande wa Ogiek kwa msingi kuwa kuchelewa huko kunazidi kukandamiza haki zao.

Dr. Dersso alisema kucheleweshwa kwa utekelezaji ni kinyume na dhana ya haki kwani jamii hiyo imekuwa ikisubiri kwa zaidi ya miaka kumi tangu kuwasilishwa kwa shauri hilo mwaka 2012 na imeendelea kuteseka tangu kufukuzwa kutoka msitu wa Mau.

Msitu huo muhimu wa Mau ulikuwa makazi ya jamii ya Ogiek kwa vizazi vingi hadi walipoondolewa na serikali ya Kenya kwa madai kuwa waliathiri mazingira ya msitu huo ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa maeneo mengi ya Kenya.

Mkurugenzi wa shirika la Ogiek People’s Development Program (OPDP), Daniel Kobei, alisema ana imani kubwa kuwa Mahakama hiyo itasimamia haki kwani tayari jamii yao ilishinda kesi lakini utekelezaji ndio changamoto iliyobaki.

Awali, mnamo Novemba 12, 2024 Mahakama hiyo iliipa serikali ya Kenya muda wa miezi mitatu kuwasilisha ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa kutii uamuzi wake wa Mei 2017 ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maamuzi hayo.

Wakati wa kikao hicho, serikali ya Kenya iliomba kuahirishwa kwa kesi ili kukamilisha ripoti ya utekelezaji, lakini upande wa Ogiek uliomba Mahakama iwalipe gharama za usikilizaji na kulalamikia mateso yanayoendelea kutokana na kutotekelezwa kwa uamuzi huo.

Kikao hicho kilikuwa cha kwanza cha aina yake chini ya Kanuni ya 81 ya Mahakama hiyo na kilihudhuriwa na jamii ya Ogiek, wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wananchi waliokuwa wakifuatilia kwa karibu hatima ya haki za jamii hiyo ya asili.