Afrika Mashariki wahimizwa kutumia bidhaa za ndani

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Riziki Pembe Juma ametoa wito kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujivunia na kutumia bidhaa zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuijenga Afrika Mashariki yenye uchumi stahimilivu na maendeleo endelevu. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akihutubia wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Kampala, Uganda

Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za Siku ya Tanzania ‘TANZANIA DAY’ katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama “Juakali”, yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo Jijini Kampala, Uganda.

“Nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali, kwa kweli bidhaa zilizopo zina ubora na ubunifu na zinavutia sana. Nitoe rai kwa wana Afrika Mashariki kutumia bidhaa hizi zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kubadilisha sekta isiyo rasmi kuwa rasmi ili wananchi waweze kushiriki katika kuchangia maendeleo endelevu na pato la Jumuiya” alisema Waziri Riziki Pembe Juma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma akifurahia muziki wa asili pamoja na wajasiriamali iliokuwa ukipigwa wakati wa maadhimisho ya SIKU YA TANZANIA kwenye maonesho ya 22 ya Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda.

Maadhimisho ya Tanzania Day yaliambatana na shughuli mbalimbali zilizofanywa na wajasiriamali wa Tanzania kwa lengo la kucherehesha maonesho na kuonesha utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. Miongoni mwa shuguli zilizofanywa ni pamoja na maonesho ya mavazi ya asili, maonesho ya vito vya thamani na madini, vyakula vya asilia, ngoma za asili na muziki.  

Akizungumza na maelfu ya washiriki wa maonesho hayo Waziri Riziki Juma Pembe mbali na kutoa wito kwa wana Jumuiya kununua bidhaa za ndani alielezea hatua mbalimbali zinazo endelea chukuliwa na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutatua changamoto zinazowakabili wajariamali, ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania amezitaja hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na; kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kuanzisha maeneo maaalum ya kufanyia biashara na kutoa elimu ya ujasiriamali.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (kulia) akiangalia bidhaa za mjasiriamali kwenye maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayoendelea jijini Kampala, Uganda

“Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kuhakikisha wajasiriamali hawa hawaendelei kubaki wadogo bali wanapaswa kukua ili waweze kushiriki katika sekta rasmi kama wajasiriamali wakubwa. Vilevile kwa kushirikia na Sekretarieti ya Jumuiya tutahakikisha maonesho haya yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwapatia fursa wajasiriamali wa sekta hii ili waweze kutambua fursa zilizopo katika nchi zetu na kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya nchi zetu”. Alieleza Waziri Riziki Pembe Juma

Hii ni mara ya tano kwa Jamhuri ya Uganda kuwa mwenyeji wa maonesho haya tokea kuanzishwa kwake mwaka 1999.