Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Yahaya Esmail Nawanda (46) kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha jiji Mwanza.

Ambapo tukio hilo lilitokea mnamo Juni 02,2024 majira ya usiku eneo la Rock City Mall, mtaa wa Ghana, wilayani ya Ilemela mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza  DCP Wilbroad Mutafungwa,amesema  jeshi hilo limefanikiwa kumkamata  Nawanda Juni  13, mwaka huu, majira ya saa 6:00 mchana, akidaiwa kutenda kosa hilo ambapo anahojiwa na taasisi za kiuchunguzi ukiwemo wa kisayansi.

“Tunamshikilia Yahaya Ismail Nawanda kwa mahojiano na upelelezi unaokwenda sambamba na uchunguzi wa kisayansi, ukikamilika jalada litapelekwa ofisi ya Mashitaka kwa hatua zaidi za kisheria ”amesema Mutafungwa.

Hata hivyo Mutafungwa ameeleza kuwa kuhusu waraka unaosambaa mitandaoni kuwa mtendewa wa ukatili huo ameamua kuondoa shauri hilo kwa hiari yake bila shinikizo la mtu yeyote na hataki kutumika kisiasa,amesema taarifa hiyo si sehemu ya uchunguzi wala ushahidi wao.

“Jeshi la Polisi tumeiona hiyo mtandaoni na matukio ya kikatili ni ya Jamhuri na mtendewa ni shahidi,taarifa hiyo ni ya mitandaoni  haikupokelewa Polisi na si sehemu ya upelelezi ”amesema.

Kamanda huyo wa Polisi amesema yanafanyika mawasiliano ya kulileta gari linalodaiwa kutumika kufanyika ukatili huo kwa sababu ni sehemu ya vielelezo vya upelelezi na wakati ukifika vitaoneshwa kama sheria inavyoelekeza.

“Uchunguzi unaendelea na tutachunguza pia umiliki wa gari hilo, vyombo vya uchunguzi vikikamilisha vitatupa taarifa kwa maandishi,”amesema.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza anayesomea Shahada ya Ugavi na Manunuzi baada ya tukio hilo  alifungua Jslada Polisi lenye namba MZR/CID//PE/74/2024,kitendo anachodai kufanyiwa katika maegesho ya magari ya baa ya The Cask eneo la Rocky City Mall ambapo inadaiwa alifanyiwa ukatili ndani ya gari lenye namba T496 BND, aina ya Toyota Crown majira ya usiku.