Na Tatu Saad,JAMHURIMEDIA

Licha ya ushindi wa bao 1-0 walioupata Taifa Stars dhidi ya Uganda katika mchezo wa kundi F kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ uliopigwa katika uwanja wa Suez Canal Authority uliopo nchini Misri,kocha Adel Amrouche amekiri kuwa wapinzani wake hawakuwa warahisi.

Adel Amrouche amefunguka kabla ya mchezo wao wa marudiano dhidi ya Uganda utakaopigwa kesho katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Adel Amrouche amesema katika mchezo uliopita wapinzani wao walijiandaa vizuri zaidi kitu kilichopelekea Taifa Stars kupata kazi kubwa sana ya kufanya ndani ya dakika 90.

“Nawapongeza wapinzani wetu Uganda kwa kujipanga vizuri maana walitupa kazi kubwa sana ya kufanya ndani ya uwanja.” Amesema Amrouche

Hata hivyo Amrouche ameahidi kuwapa furaha watanzania, wapenzi wa soka na wote waliowapa ushirikiano katika mchezo wao wa kwanza.

“Naahidi nitafanya kila kitu kwa uwezo wangu kuhakikisha tunawapa furaha Watanzania na wale wote waliotupa sapoti yao kwenye mchezo huu.” Amesema Amrouche

Stars imefikisha alama 04 katika msimamo wa Kundi F, na inahitaji ushindi mwingine dhidi ya Uganda kesho Jumanne (Machi 28) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ili kuzisogelea fainali za AFCON 2023 zitakazopigwa huko Ivory Coast.

By Jamhuri