Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,

IKIWA leo ni Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani asilimia 16 ya watu waliofanya uchunguzi katika kambi ya uchunguzi ya siku mbili wamegundulika kuwa na tatizo hilo.

Kambi ya uchunguzi iliyoanza Mei 16 na 17,2024 ilihudhuriwa na watu 2014, ambapo kati yao asilimia 16 walikuwa na shikizo la juu la damu.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Tatizo Waanne amesema watoto waliofanyiwa uchunguzi ni 32 ambapo kati yao 16 walikutwa na matatizo ya kiafya.

“Leo ni siku ya shikizo la juu la damu  ambapo magonjwa ya moyo yanachangia vifo vyote duniani kwa asilimia 30 hususani shinikizo la damu, huu ni ugojwa ambao kama una mtindo bora wa maisha unaweza kuzuia visababishi,”amesema.

Dk Waanne amesema mtu anapopatikana na tatizo anaweza kupata madhara katika mwili kama moyo kuwa mkubwa, kiharusi,matatizo ya figo huku sababu kubwa ni shikizo la damu.

“Kambi hii ni muhimu kama tungekuwa hatujafanya hawa watu wasingejua na sasa wanaweza kuchukua hatua.

Ameeleza kuwa visababishi havijulikani lakini tafiti zinaonesha wanaokunywa pombe kupita kiasi wanaweza kupata, matumizi ya bidhaa za tumbaku kama ugoro, shisha,s igara, kutokufanya mazoezi, ulaji usiofaa na uzito mkubwa.

“Tuna kambi ya matibabu mara kwa mara ili kufikia wananchi wengi zaidi na tuna wataalmu wengi wanashiriki na zoezi ni endelevu kila baada ya muda fulani tunafanya, nawashauri watu wawe na tabia ya kupima afya na kubadili mtindo wa maisha kwa sababu matibabu haya ni ghali ,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mkazi wa Temeke Mikoroshini, Hamisi Gadawi amesema anashukuru kwa kupata huduma za vipimo na dawa bure kwani angeenda kwingine angetoa fedha.

Naye Chusiku Sulemani amesema kuwa amegundulika na kisukari na shinikizo la juu la damu na madaktari wamemshauri vyakula anavyotakiwa kula.