Balile:Bado kuna vifungu vya sheria ambavyo ni kandamizi’

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri (TEF),Deodatus Balile amesema kuwa bado kuna maeneo katika vifungue vya sheria ya habari vimekuwa vikwazo na vinahitaji kufanyiwa marekebisho.

Hayo ameyasema jana katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na Televisheni ya ITV kuhusiana na Marekebisho ya sheria ya huduma ya habari.

Balile amesema kuwa madhumuni makubwa ya mahitaji ya kupitia marekebisho ya sheria ya huduma ya habari 2016 ni kuona jinsi gani ya kuwa na sheria nzuri ya kuwahudumia Watanzania.

“Mwananchi akiwa amezaliwa ana haki ya kuishi hivyo haki za msingi inawezesha haki zingine kupatikana kwa maana kwamba mwananchi akiwa anakula analala bila kupata taarifa hatoweza kuendelea na wala kufahamu chochote na pia hatopata maendeleo, hatolipa kodi wala kuendeleza nchi yake kwa matokeo hayo anaweza kuwa kuishi kama zoo ya wanyama.

“Mwanadamu kuishi kwa kubadilishana mawazo kutoka sehemu moja kwenda nyingine anakuwa na uelewa mpana, pia anakopa mawazo na kwenda kuyafanyia utekelezaji hivyo yanaleta maendeleo kwake na hata kwa taifa.

‘Mwananchi ana haki ya kusikilizwa, haki ya kupata habari hivyo tunapozungumzia uhuru wa vyombo vya habari si kwa ajili ya waandishi peke yako bali tunapigania haki za wananchi waweze kupata haki ya kusikilizwa na kupata habari.

‘Sheria inayoongoza huduma za habari ilingia Julai 22,1920, wakati huo Mwingereza aliamua kuileta hapa nchini wakati huo kulikuwa na kaubauguzi fulani kwa Mwafrika ikiwa ni pamoja na asipate taarifa sahihi hata mfumo wa elimu pia ulikuwa ni kujua kusoma, kuhesabu na kuandika,’ amesema.

Ameongeza kuwa nia ya kudai haki si kutaka kushindana wala kupendelea isipokuwa kuwezesha haki nyingine kupatikana mfano tu akienda hospitali na ananyikwa haki ya kupata matibabu ama anadaiwa rushwa aje kwenye vyombo vya habari azungumze.

“Hivyo tunapodai haki si kwa ajili yetu bali ni kutafuta haki ya kuwezesha haki nyingine kupatikana na kwa faida ya wananchi na faida taifa letu,” amesema.

“Katika sheria ya 1976 kuna mambo yalibadilishwa na yapo yaliyobaki ambayo ni kikwazo mfano ni kifungu cha 25 ambapo kinampa mamlaka ambaye ni waziri kufungia au kulifuta gazeti lolote,hivyo kwa sheria hiyo inafanya waziri kuwa mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mtoa hukumu.

“Anaweza kaamka asubuhi akaamua kulifungia gazeti kwa siku 90 hujui kosa ni nini na je amezungumza na wahusika hapa ndipo tunapoona kuwa panahitaji marekebisho ya sheria na tuwe na utawala wa sheria.

“Tulikubaliana kuwa twende katika misingi inayokubalika kimataifa na ilipotolewa uamuzi wakaondoa neno waziri likawekwa neno Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),kitu ambacho ni kile kile,” amesema.

Balile amesema kuwa kwa mtazamo huo imekuwa kikwazo kwa wana habari jambo ambalo wamekuwa wakikipigia kelele kifungu hicho kufanyiwa marekebisho kwani kinawanyima uhuru vyombo vya habari.

Afisa Uchechemuzi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Raymond Kanegene amesema kuwa taarifa ni kitu cha msingi katika jamii hata dunia imeweka ibara ya 19.

Pia kuna mkataba wa haki za binadamu 1981 kuanzia hatua ya kimataifa na nchini mwetu katika katiba yetu ya 1977 ibara ya 18 inazungumzia mtu kupata habari, kutafuta habari na kusambaza.

Amesema kuwa kwa namna ambavyo wameangalia kuanzia 1920 hadi sasa kwa mabadiliko ya ulimwengu kwa kuanzia 2016 Tanzania imeonekana kama uhuru wa habari kuanza kushuka.

“Kama wadau wa haki za inadamu anaona ipo haja ya kuangalia baadhi ya hivyo vifungu kwa kufanyiwa marejebisho kwani wananchi wengi wanatumia vyombo vya habari kufikisha malalamiko hayo kwani kwa kufanya hivyo kunaongeza uwajibikaji,” amesema.