Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

BENKI ya NMB imeanzisha mpango maalum wenye masuluhisho mahususi kwa ajili ya kuwahudumia wastaafu na wastaafu watarajiwa unaoitwa NMB Hekima Plan.

Utaratibu huu ambao lengo lake kubwa ni kusaidia kuenzi mchango mkubwa wa watumishi hawa katika ujenzi wa taifa umezinduliwa rasmi Oktoba 16, 2023 jijini Dodoma wakati wa warsha maalum kwa ajili ya kuwaelimisha kifedha na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya ajira.

 Mgeni rasmi katika uzinduzi wa programu hiyo mpya ambayo kauli mbiu yake ni “Staafu Kifahari” alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako.

 Katika hotuba yake, kiongozi huyo amebainisha kuwa mashuruhisho hayo na programu yake ya elimu ni wazo kubwa na mtambuka katika jitihada za Taifa kuboresha maisha ya wazee wote nchini.

Ameongea kuwa pia ni suala la thamani kwa azma ya Serikali ya kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuhakikisha kuwa wastaafu si tu wanaishi maisha bora na ya furaha lakini pia kuhakikisha wanaendelea kuchangia juhudi za ujenzi wa taifa.

 “Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchni ili wastaafu waweze kuchangamkia fursa zinazoletwa na taasisi za fedha kama huu mpango wa NMB Hekima Plan,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akizindua rasmi mpango maalumu kwaajili ya wastaafu na wastaafu watarajiwa wa Benki ya NMB uitwao NMB Hekima Plan katika hafla maalum iliyofanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma. Watatu kushoto ni Mkuu wa idara ya Huduma za Serikali wa Benki ya NMB, Vicky Bishubo na watatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri. Wengine ni Mkuu wa Idara ya mtandao wa matawi na Mauzo wa Benki ya NMB, Donatus Richard (wapili kushoto), mwakilishi wa wastaafu, Mzee Martine Chiwaligo (wapili kulia), Meneja wa Benki ya NMB kanda ya kati, Janeth Shango (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa benki hiyo, Aikansia Muro (kulia).

Akisisitiza umuhimu wa wastaafa kuwa na nidhamu ya fedha na matumizi ya pensheni zao, waziri huyo amebainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali kuiimarisha sekta hiyo ni pamoja na kuboresha mifuko ya hifadhi ya jamii na utoaji wa huduma kwa ujumla.

 Hii ni pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa cha madeni ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kupitia hatifungani maalum ambayo mwaka 1999 yalikuwa ni jumla ya Sh trilioni 4.6.

 “Serikali pia imefuta kiasi kikubwa cha madeni yake kwa PSSSF kwa kulipa Shilingi bilioni 500 kati ya Shilingi bilioni 982 ilizokuwa inadaiwa,” Prof Ndalichako aliwaambia wastaafu zaidi ya 400 wa Dodoma walioshuhudia uzinduzi wa programu hiyo.

 Aidha, amesema uwekezaji unaofanywa kubuni masuluhisho ya kidijitali na michango ya wadau kama Benki ya NMB yatasaidia si tu kuwahudumia wastaafu lakipi pia upatikanaji wa huduma kwa watu wote.

 Ameongeza kuwa yeye binafsi na Serikali kwa ujumla wanatambua changamoto za kifedha ambazo wastaafu mawekuwa wakikumbana nazo ikiwemo  kukosa uwezo wa kupangilia mapato na matumizi ya fedha zao, kupungua kwa kipato cha mwezi, kukosa usalama wa fedha pamoja na nyingine nyingi za kimaisha.

“Niwasihi washiriki wa warsha hii na wastaafu wengine kuzingatia mafunzo na maarifa mtakayopewa na wataalum ili muweze kuzikabili changamoto hizi,” amesema

 Katika maelezo yake kuhusu programu nzima ya masuluhisho hayo, Mkuu wa Idara ya Huduma na Biashara wa benki hiyo, Bi Vicky Bishubo, alinena maneno yafuatayo; “Tumekuwa benki kiongozi katika kila kitu na kwenye kutoa huduma bora kwa wastaafu na tunaendelea kuboresha huduma zetu kwa ajili yao kupitia maarifa na rasilimali fedha,” amesema

 Aidha, amesema masuluhisho yaliyomo kwenye NMB Hekima Plan ni pamoja na mikopo mbalimbali ikiwemo ile ya nyumba ambapo mkopaji anaweza kupata hadi Shilingi bilioni 1.

Kupitia utaratibu huu wastaafu watapewa pia elimu ya ustawi wa afya na usalama wa fedha zao huku wakionyeshwa fursa mbalimbali za uwekezaji.

 Afisa huyo mwandamizi alisema NMB Hekima Plan ina na bima za afya na mali za gharama nafuu na bei shindani sokoni.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana Ajira na wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akizindua rasmi mpango maalumu kwaajili ya wastaafu na wastaafu watarajiwa wa Benki ya NMB uitwao NMB Hekima Plan katika hafla maalum iliyofanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma. Wapili kushoto ni Mkuu wa idara ya Huduma za Serikali wa Benki ya NMB, Vicky Bishubo na wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri. Wengine ni Mkuu wa Idara ya mtandao wa matawi na Mauzo wa Benki ya NMB, Donatus Richard (kushoto), mwakilishi wa wastaafu, Mzee Martine Chiwaligo (kulia)

 Zipo pia akaunti maalumu zisizokuwa na makato ya mwezi ambazo zinampa nafasi mstaafu kupata mkono wa pole wa hadi Sh milioni 2 endapo yeye au mwenza wake atafariki na kumwezesha kupata kiasi kama hicho akipata ulemavu wa kudumu.

Bishubo aliwaambia washiriki wa warsha hiyo kuwa baada ya uzinduzi wa programu ya NMB Hekima Plus, zoezi la kutoa elimu litafanyika nchi nzima.

“Tutambue pia uwepo wa wastaafu watarajiwa ambao nao wameungana nasi siku ya leo. Tumeona ni vyema tuwaalike kwani ni kundi ambalo wataingia katika kustaafu muda si mrefu na ni vyema wakaanza kuandaliwa mapema kukabiliana na maisha ya kustaafu,” aliongeza.

 Aidha alibainisha kuwa NMB inaamini programu hizi zitaondoa ile hofu ya kustaafu kwa baadhi ya watumishi kwani watakuwa wameandaliwa kikamilifu kuishi vyema baada ya utumishi.

By Jamhuri