Serikali yakanusha uvumi kuhusu uwepo wa kiwanda cha kutengeneza mayai Goba


Muonekano wa mayai ya kuku ambayo mawili yanaonekana yakiwa na umbo dogo zaidi tofauti na umbo la kawaida ambapo inaelezwa mayai hayo yanatoka kwa kuku wa kawaida na huwa yanatotolewa kutokana na sababu mbalimbali na hayana madhara ya kiafya kwa matumzi ya binadamu. (16.10.2023)

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakanusha taarifa za uwepo wa kiwanda cha kutengeneza mayai katika Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii. Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa imefuatilia suala hilo kwa kina na kujiridhisha kuwa tarifa hizo sio za kweli, ni upotoshaji na hivyo kuitaka jamii  kuipuuza.

Kuanzia tarehe 12 Oktoba 2023 kumekuwa na picha ya mayai mengi na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa kiwanda cha kutengeneza mayai katika Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam. Picha hiyo imeambatana na maneno “Serikali Hailali Kama alivyo Shetani Halali!! Wanajua kabisa Kwa sababu Shetani Halali kwa hiyo Kuna Mambo Mabaya atayatenda tu!! Kiwanda Cha mayai Goba Kwa wachina kimekamatwa Sasa hayo Mayai Yote Sijui yametagwa na Kuku Gani? Tusubiri yanayojiri, Usikie Technologia ilivyo hapo Ndiyo utakapojua Kwa nini kila Mtu Ana Kitambi”.

Taarifa hizo zimetengenezwa kwa nia ovu ya kuharibu tasnia ya kuku nchini inayokuwa kwa kasi. Katika kufuatilia zaidi, Wizara imebaini kuwa picha hiyo ya mayai mengi iliyotumiwa ilionekana kwenye mitandao ya kijamii mwaka 20.16 na haikupigwa hapa nchini

Vilevile, kuna kipande cha video (video clip) ya kijana anauza mayai ya kuchemsha ambayo yana viini viwili ambapo baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii wanasema mayai haya yanatengenezwa viwandani na yanaweza kuwa hatarishi kwa afya ya binadamu. Mayai yenye viini viwili hayatengenezwi viwandani bali yanatagwa na kuku kama kawaida. Sababu zinazopelekea yai kuwa na viini viwili ni pamoja na:

  • Umri wa kuku, mara nyingi hutokea kwa kuku wanaoanza kutaga au wanaomalizia umri wa kutaga;
  • Chakula: Wakipewa chakula chenye virutubisho vingi kuku huweza kuwa na mayai yenye viini viwili;
  • Kuwasisimua kuku kwa mwanga (overphotostimulation);
  • Aina ya kuku (genetic effects).

Viini viwili kwenye kuku ni sawa na ilivyo mapacha kwa wanyama wengine. Kinachotekea hapa ni kuwa kampuni za vitotoleshi vya vifaranga hazipendelei kutumia mayai yenye viini viwili kwa kuwa mayai haya huwa mara nyingi hayaanguliwi, au hata yakianguliwa vifaranga vitakavyopatikana vinakuwa na uzito mdogo sana au vinakuwa na ulemavu. Hivyo, kampuni hizo huyabagua mayai yote yenye viini viwili na kuyauza kama mayai ya chakula kama ilivyoonekana kwenye kipande cha video. Nipende kuwatoa wasiwasi walaji wa mayai haya kuwa ni salama kwa matumizi ya binadamu. 

Naomba kumalizia kuwa uzushi uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa uwepo wa taarifa ya kiwanda cha kutengeneza mayai ni upotoshaji na unapaswa kupuuzwa. Serikali inafuatilia kwa kina aliyeanzisha uhalifu wa taarifa hii na akipatikana Sheria itachukua mkondo wake.

Prof. Hezron Emmanuel Nonga

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo,

Wizara ya Mifugo na Uvuvi,

Simu: 0767238174

Barua pepe: [email protected]

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akikagua uzalishaji wa mayai kwa Esther Ng’amilo ambaye ni mmoja wa wafugaji wakubwa wa kuku wa mayai katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.