Bomoabomoa yazikumba nyumba 152 Pwani, wakazi wajihifadhi shuleni

Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Kibaha

Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, ametolea ufafanuzi sakata la bomoabomoa ya nyumba katika kitongoji cha Matuga, Kata ya Kawawa na Zegereni wilayani Kibaha na kusema endapo kama hawajaridhika na maamuzi ya Baraza la Ardhi Wilaya ,wafuate utaratibu wa kisheria kukata rufaa ama wapate zuio la Mahakama ya Mkoa Pwani kwani utekelezaji huo haujakurupushwa bali umetekelezwa kwa mujibu wa sheria.

Kunenge ameeleza Serikali ya mkoa wajibu wake ni kushughulika na yale ambayo wana wajibu nayo ili kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama umaimarika na pia utekelezaji wake unafanyika kwa mujibu wa sheria na si kuingilia maamuzi ya mhimili wa Baraza la Ardhi ama mahakama.

Baadhi ya nyumba zilizobomolewa kama zinavyoonekana pichani.

Akitolea ufafanuzi juu ya bomoabomoa, Kunenge ameeleza Serikali ya mkoa inafahamu na kwamba nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na katiba ina mihimili mitatu Mahakama, Serikali na Bunge.

“Mihimili hii inafanya kazi bila kuingiliwa ingawaje mihimili hii inashirikiana ,inapotokea migogoro mbalimbali mfano upande huu wa ardhi, migogoro hii inaweza kutatuliwa kiutawala ,lakini pia inaweza kutatuliwa kisheria kwa kwenda katika mahakama na kwa mujibu wa sheria zetu migogoro inaweza kutatuliwa katika mabaraza ya ardhi ya wilaya na mahakama “amefafanua Kunenge.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson John alipoulizwa juu ya mgogoro huo ambao inadaiwa mmiliki halali wa eneo hilo ni Omari Kadri ,katika hukumu iliyotolewa katika kesi namba 176/2022 na kufunguliwa dhidi ya wadaiwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Zegereni na Baltazar Saimon ambapo amesema kuwa zoezi hilo limetokana na amri ya Mahakama,kama wapo walioguswa na hukumu wana haki ya kukata rufaa.

Naye Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Constantino Mwakamo alifika kutoa pole kwa wahanga na kusema walioguswa na bomoabomoa hiyo watafute utaratibu wa zuio ama rufaa.

“Kesi hiyo ilitambulika baina ya mmiliki Kadri dhidi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Zegereni pamoja na Bartazar Saimon lakini cha kustaajabisha katika maamuzi wameingizwa na maeneo mengine ya Matuga,Kawawa ambao hawakuhusika kwenye kesi.

“Kinachoshangaza ni huyo Kadri kwenye kesi yake hawakuwepo wakazi wa Matuga sasa imekuwaje waingizwe katika maamuzi ya kubomolewa tena bila kupewa notisi ya kubomolewa wala kupewa taarifa”amefafanua Mwakamo.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa kijiji Cha Matuga ,Jofrey Kazinduki ameeleza hadi sasa eneo la Matuga pekee wameshabomolewa nyumba takriban 152 kati ya hizo nyumba za kisasa ni 131 na za vibanda vya kawaida 21.

Ameeleza,kwa sasa wahanga wanaishi kwa majamaa,ndugu wengine wamejihifadhi shuleni kusubiri hatma yao na kuongeza wanashindwa kwenda kuweka zuio kwakuwa hawajawahi kushtakiwa na kesi haikuwataja zaidi ya Zegereni hivyo kutokana na Serikali mkoa kuwapa ushauri watakwenda mahakama ya mkoa kutoa malalamiko yao.

Happy Festo mama wa watoto wanne mkazi wa kijiji cha Matuga amesema alikuwa akiishi hapo baada ya dada yake kumpatia eneo ili aishi na watoto kulingana na ugumu wa maisha ,alibainisha kwa sasa yupo kwenye hali ya sintohamu kwani hana pa kuishi zaidi ya kujihifadhi kwenye banda la kuku.

Ameiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ambao wana watoto na ambao hawana msaada wowote kwani hata kama haiwezi kuingilia mhimili mwingine kisheria waangalie usalama wa raia na kuwa nao karibu.