Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam

Ndugu wa Marehemu Robart Mushi (34) maarufu kwa jina la Babu G wamekanusha taarifa za uongo na uzushi zinazosambaa katika mitandao ya kijamii iliyoambatanishwa na picha yake na kupitia Account ya Boniface Jacob na Malisa GJ ikituhumu Jeshi la Polisi kuhusika na kifo cha mtu huyo .

Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo shemeji wa marehemu Gunda Asheri amesema ndugu yao walimtafuta tangu Aprili 10, 2024 siku ya Sikukuu ya Iddi na walizunguka katika hospitali zote mochwari lakini siku ya juzi kupitia Azam Media waliona kuna mwili wa uliokotwa maeneo ya Matumbi.

Ameaema kuwa ndugu waliamua kufuatilia eneo hilo kisha kuzungumza na watu wanaofanya shughuli zao wakaambiwa wanaohusika kufanya doria ni Polisi kituo cha Tabata walienda katika kituo hiko wakaambiwa ni kweli kuna mwili uliokotwa eneo Matumbi darajani na mwili umepelekwa Hospitali ya Barac Kilwa Road hivyo wakapelekwa sehemu ya kuhifadhia miili wakakagua na kubaini mwili wa marehemu na wakapewa taratibu namna na kuupata mwili huo kwa shughuli ya kuuhifadhi.

” Cha kilichotushtua sana jana ni kuona taarifa zikienea katika mitandao ya kijamii zimepostiwa kwenye ukurasa wa Boniface Jacob kiukweli hatukuridhishwa na taarifa hizi kuchafua Jeshi la Polisi na sisi familia hatuhusiki kabisa na taarifa hizo sisi tumepewa maelezo yote juu ya kifo cha ndugu yetu kwa askari wa Jeshi la Polisi usalama barabarani wa eneo hilo(Trafic police) na mwili tulivyoouona unaonekana aligongwa na gari wakati akivuka barabara ” amesema ndugu wa marehemu

Aidha Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro ametoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa ya uongo na uzushi inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha Robart Mushi @ Babu G ambaye picha yake imeambatanishwa kwenye taarifa hizo amesema mtu huyo alipotea Aprili 11, 2024 na baadae kugundulika katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road huku ikidaiwa Polisi kuhusika na kifo hicho kwa kumuua.

“Ukweli ni kwamba tarehe 11 Aprili, 2024 majira ya saa 10 alfajiri askari Polisi wa Usalama barabarani alipewa taarifa na mwananchi wa eneo laTaa za kuongozea magari za Buguruni, Ilala mtu mmoja mwanaume aliyekuwa akivuka barabara eneo hilo la Kimboka kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama (hit and Run) mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani, kifuani na eneo la chini la mgongo na kisigino cha mguu wa kulia” amesema Kamanda.

Hata hivyo eneo hilo lina watu wengi ambao wanakesha kwa biashara mbalimbali na walishuhudia tukio hilo na mtu huyo alipelekwa haraka Hospitali ya Amana na Polisi lakini baada ya kumfikisha madaktari walibaini kuwa mtu huyo alikuwa tayari amekwishafariki.

Ameaema kuwa kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Amana kilikuwa hakina nafasi, ilishauriwa akahifadhiwe kwenye Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyo barabara ya Kilwa Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia kuhusiana na suala hilo.

Hivyo Aprili 21, 2024 ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili wa ndugu yao kwani hakuwa na kitambulisho wala simu. Taratibu za mwisho za mazishi zinafanywa ili akazikwe.

Kutokana na taharuki iliyotengenezwa na kujengwa kwa makusudi na mtu anayejiita Malisa GJ na Bonoface Jacob ambao kwenye “post” zao walionesha nia ya wazi ya kutengeneza chuki dhidi ya Polisi na Serikali kwa wananchi kuwa mtu huyo aliyepata ajali alikuwa ameuawa na Polisi ,kitendo kilichofanywa na watu hao ni kosa kisheria na hakivumiliki na lazima jeshi lichukue hatua za kisheria dhidi ya wahusika ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwahoji kwa kina kisha kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.

Jeshi la Polisi halitavumilia watu ambao wanaibuka na taarifa za uongo na uzushi ambazo zinalenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi.

Jeshi litaendelea kusimamia misingi ya kisheria na halitakuwa na huruma kwa mtuhumiwa yoyote wa kihalifu na litamshughulikia haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa sheria.

By Jamhuri