Na Mwandishi Wetu

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kimezindua klabu ya ujasiriamali kwa shule ya sekondari Temeke Wailes iliyoko Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi wa klabu hiyo ulifanyika jana Ijumaa kwenye shule hiyo.Chuo hicho kimesema vilabu hivyo vinalenga kuwawezesha wanafunzi kukua wakifahamu masuala mbalimbali ya biashara tangu utotoni ili waweze kuwa wajasiriamali siku za mbele.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hiyo Mkurugenzi wa Shahada za Juu, Tafiti na Ushauri wa chuo hicho, Dkt. Tumaini Ubadius, amesema wanalenga kuzifikia shule zote za Dar es Salaam.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Wailes iliyoko Temeke jijini Dar es Salam wakionyesha utaalamu waoa wa kutengeneza sabuni shuleni hapo mbele ya viongozi kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), walipoenda shuleni hapo kufungua klabau ya ujasiriamali

Dk.Tumaini amesema chuo hicho kimeona ni muhimu wanafunzi wakaanza kufundishwa kuhusu ujasiriamali wakiwa wadogo ili wanapohitimu elimu ya juu wawe na uelewa mpana kuhusu masuala ya biashara.

Amesema kupitia mpango huo, chuo kitakuwa kikipeleka walimu wake kila siku ya Alhamisi kwaajili ya kufundisha wanafunzi wanaosomea mchepuo wa biashara masuala ya ujasiriamali.

“Tunataka kupunguza tatizo la watu kutafuta ajira ili wanapomaliza masomo yao waweze kujiajiri na tunachofanya ni kukuza vipaji na ubunifu walionao tangu wakiwa wadogo,” amesema.

“Tumeona tuanze kuwajengea uelewa kuanzia huku chini ili kijana anapokuwa aweze kuwa na ufahamu mazingira yanayomzunguka na changamoto zinazomzunguka kuwa fursa kwake kwa kusaidia jamii na kujiingizia kipato,” alisema

Wanafunzi wa shule ya sekondari Temeke Wailes jijini Dar es Salam wakiimbia wimbo wa taifa kabla ya uzinduzi wa klabu ya ujasriamali iliyozinduliwa shuleni hapo mwishoni mwa wiki na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Amesema wamepanga kutembelea shule zote za Dar es Salaam na kuanzisha klabu kama hizo lakini wataenda kwenye mikoa ambayo CBE ina kampasi zake kama Mbeya, Mwanza, Dodoma na Zanzibar.

Mkuu wa shule hiyo, Catherine Mdachi aliushukuru uongozi wa CBE kwa kuichagua shule hiyo kuwa miongoni mwa shule za mwanzo kuwa na klabu hiyo.

“Kuna mkuu wa shule moja alinipigia simu kuniambia hivi kwanini hao CBE wameamua kuja huko na kuja huko kwenu nikawaambia ni habati yetu,” amesema

Mwalimu Mkuu wa shule ya Temeke Wailes, Catherine Mdachi na Mkurugenzi wa Shahada za Juu, Utafiti na Ushauri wa  wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),dk. Tumaini Ubadius, wakikata keki kuashiria uzinduzi wa klabu ya ujasiriamali shuleni hapo mwishoni mwa wiki

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutujengea madarasa ili watoto wetu wapate sehemu ya kusoma, Huku Temeke hatujui nyota ya kijani tuna watoto wengi lakini tunamshukuru mama ametujengea madarasa mengi,”

Amesema uamuzi huo wa CBE umekuja wakati muafaka kwasababu kuna tatizo kubwa la ajira kwa hiyo kuwafundisha wanafunzi ujasiriamali kutawasaidia kujiajiri kwa kuanzisha biashara zao.

By Jamhuri