Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa Mikataba na Hati za Makubaliano ya kimkakati 15 akiwa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping. 

Miongoni mwa mikataba hiyo iliyolenga kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji wa baina ya nchi hizo mbili umeshuhudia China ikiipunguzia Tanzania sehemu ya deni lake la thamani ya Shilingi Bilioni 31.4. 

Miongoni mwa mikataba na makubaliano yaliotiwa saini ni kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la usafirishaji wa maparachichi kutoka Tanzania kwenda China. 

Pia wametia saini Mkataba unaohusu msaada wa RMB milioni 100 za ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu baina ya nchi hizo mbili.

Vile vile, kumetiwa saini makubaliano kuhusu mahitaji ya kuwepo na soko kubwa la Usafirishaji wa Mabondo ya Samaki pamoja na bidhaa nyingine za uvuvi kutoka Tanzania kwenda China. 

Aidha, China imetoa mkopo wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 56.72 wenye masharti nafuu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar, Terminal II. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping wakati Wimbo wa Taifa wa Tanzania ukipigwa kwenye ukumbi wa The People Great Hall, Beijing nchini China tarehe 03, Novemba, 2022.

China inaongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania. Hadi kufikia Mwezi Oktoba 2022, Jumla ya miradi 1,098 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 9.6 ilisajiliwa katika kituo cha uwekezaji cha TIC.  

Miradi hiyo imezalisha ajira 131,718. Uwekezaji huo umefanyika katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano, madini na uvuvi. 

Rais Samia yupo nchini China kwa ziara ya Kiserikali kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais wa nchi hiyo ambapo pia alikutana na kuzungumza na  Waziri Mkuu wa China pamoja na Spika wa Bunge la nchi hiyo.  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping wakati akikagua Gwaride la Heshima katika ukumbi wa The People Great Hall, Beijing nchini China tarehe 03, Novemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa The People Great Hall, Beijing nchini China tarehe 03, Novemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo ya pamoja na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping, Beijing nchini China tarehe 03, Novemba, 2022.

By Jamhuri