Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Mkuranga
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini (CTI) ,limempongeza Rais Samia kwa kuwapa fursa kubwa wafanyabiashara ya kukaa nao meza moja ya majadiliano kuhusu namna ya kutatua changamoto zao.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga wakati akizungumza kwenye kiwanda cha Lodhia Industries cha Kisemvule Mkuranga kinachozalisha nondo, mabati na bidhaa za plastiki.
Alikuwa akizungumza wakati ujumbe wa CTI ulipotembelea kiwanda hicho kuangalia uzalishaji na changamoto za kiwanda hicho.
Tenga alisema Rais Samia anataka kuona uwekezaji unaongezeka na viwanda vinajengwa kwa wingi na kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazomudu kuingia kwenye masoko ya kimataifa hivyo kusaidia kukuza uchumi.
“Siyo siri sisi CTI tunafurahia kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kupigia debe uwekezaji wa viwanda na kuhitimiza sekta binafsi kufanya hiyo kazi,” alisema Tenga
Alikipongeza kiwanda hicho kutokana na uwekezaji mkubwa walioufanya na kusababisha ajira nyingi kwa watanzania.
Tenga alisema bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda hicho yakiwemo mabati, nondo na plastiki ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi kwani ujenzi wa miundombinu unategemea kuwepo kwa bidhaa hizo.
“Unapojenga barabara, madarasa, madaraja na miundombinu yote unahitaji chuma kwa kiasi kikubwa sana sasa sisi tunajisikia fahari sana kuona mwanachama wetu Lodhia amewekeza kwa kiwango kikubwa kama mnavyoona wenyewe,” alisema Tenga
“Lodhia anatekeleza maono ya serikali ya awamu ya sita ambayo siku zote inasisitiza na kuhamasisha uwekezaji kupitia ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa kama hivi vya nondo na plastiki na tunafurahi zaidi kuona mwekezaji huyu ni mtanzania,” alisema Tenga
Aidha, Tenga aliwaomba watanzania kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani kwa kununua bidhaa zao kwani zina ubora wa kimataifa na wakati mwingine zinazidi viwango vya baadhi ya bidhaa za nje.
“Bidhaa hizi zina ubora wa hali ya juu na nitafurahi kama nitaona watanzania wanachangamkia bidhaa za viwanda vya ndani zikiwemo za nondo, mabati na plastiki kutoka Lodhia ili kuendelea kulinda ajira za watanzania ambao wamepata ajira,” alisema
Tenga aliomba serikali na taasisi zake kuendelea kununua bidhaa za viwanda vya ndani zikiwemo ndono na bidhaa za plastiki zinazozalishwa na kiwanda cha Lodhia kama sehemu ya kulinda viwanda vya ndani.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda hicho, Manoj Gopi, aliomba serikali kuweka mkakati kabambe kulinda viwanda vya ndani kama zinavyofanya baaadhi ya nchi jirani kwa kuhakikisha zinanunua kwa wingi bidhaa kutoka kwenye viwanda hivyo.
Alisema hatua hiyo itasaidia kukuza viwanda hivyo na kuongeza nafasi za ajira kwa watanzania wengi wanaofanya kazi kwenye viwanda hivyo na kulinda hifadhi ya dola ambayo imekuwa ikitumika kuagiza bidhaa nje ya nchi.
Alisema bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho zimekidhi vigezo vyote vya kimataifa hivyo haoni sababu yoyote kwa serikali kuendelea kuagiza bidhaa za nje kwaajili ya kutekeleza miradi yake ya miundombinu.
Aidha, alisema wamekuwa wakiuza nondo kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali ukiwemo ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi, bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere Rufiji Mkoa wa Pwani na miradi mingine ya barabara.
“Wenzetu Kenya wameweka sheria kali sana za kulinda viwanda vyao na Uganda wamefanya hivyo hivyo sasa na hapa kwetu kuna umuhimu wa kuendelea kulinda viwanda kwa kuacha kuagiza nje bidhaa kama nondo na bidhaa za plastiki ambazo zinazalishwa hapa nchini na zina viwango vya kimataifa,” alisema
Aidha, alisema Lodhia Industries inawekeza dola za Marekani milioni 60 kwenye ujenzi wa kiwanda cha mabati katika eneo hilo ambacho kinatarajiwa kuanza kuzalisha mabati kuanzia mwezi Mei mwaka huu kitakachotoa ajira zaidi ya 500 za moja kwa moja.
Alisema kwenye kiwanda cha nondo na bidhaa za plastiki wamewekeza dola za Marekani milioni 45 na kuwezesha ajira zaidi ya 2,000 za moja kwa moja.
“Uwekezaji huu ni mkubwa sana tunaomba serikali iweke mikakati ya kutulinda na kutupa kipaumbele kwa kununua bidhaa zetu, serikali inapigia debe viwanda kwasababu ndivyo vinakuza uchumi na kuongeza ajira,” alisema
Aliomba taasisi za serikali kama Shirika la Viwango nchini TBS na Tume ya Ushindani FCC kufanyakazi kwa karibu na viwanda hicho kuhakikisha kunakuwa na biashara ya ushindani dhidi ya bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Lodhia inaviwanda 15 hapa nchini sasa unaweza kuangalia tumeajiri watanzania wangapi kwa hiyo kukua kwa viwanda vyetu ni afya kwa uchumi wa nchi na kadiri tunavyokuwa ndivyo tunazidi kuongeza ajira kwa watanzania wenzetu,” alisema