Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imefanya kikao Maalum tarehe 15 Januari, 2024, Zanzibar, chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Katibu Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Itikadi na Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda imesema kuwa kikao hicho kilitanguliwa na semina kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuanzia tarehe 13 – 14 Januari, 2024.

Wajumbe walipewa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wake ikiwemo mradi wa Bwawa la Umeme wa Julius Nyerere (JHPP) na mipango ya kuboresha hali ya umeme nchini.

Mradi wa Reli ya “Standard Gauge Railway (SGR)”, Ujenzi wa daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo – Busisi), Utekelezaji wa Ilani ya CCM, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hali ya Mashirika ya Umma Nchini na Mageuzi yanayohitajika.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipokea taarifa mbalimbali ikiwemo: Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka 2024, Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 47 ya Kuzaliwa kwa CCM.

Aidha, kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kimepokea pendekezo la Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuhusu jina la Katibu Mkuu wa CCM.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa wameridhia kwa kauli moja pendekezo hilo na kumchagua Balozi (Mst) Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kimeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Ndugu Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 kwa upande wa Zanzibar na kufanikisha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Vile vile, kikao hicho kimepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

By Jamhuri