Kutoka kuuza kahawa Kariakoo hadi chapuo la kuwa mbunge (3)
 
TABORA

NA MOSHY KIYUNGI


Wiki iliyopita tuliona jinsi Harmonize alivyoweza kutunga nyimbo na kuzifanya akiwa peke yake, lakini pia alikuwa mkali wa kushirikisha wengine kwenye nyimbo zake kama ambavyo na yeye alivyoshirikishwa na wanamuziki wengine.
Hadi kufikia hatua hiyo, tayari Harmonize alikuwa ameshafanikiwa kujijengea jina kubwa katika tasnia ya muziki, si tu nchini, bali hata nje ya mipaka ya nchi. Tulielea awali kuwa jina lake halisi ni Rajab, lakini anatambulika zaidi kwa jina la Harmonize na watu wengi hawalifahamu jina lake halisi. Ni nini asili ya jina hili la kimuziki?
Harmonize anasema alipewa jina hilo na producer wa Record Lebel pamoja na mashabiki wake.
Harmonize alifika jijini Dar es Salaam mwaka 2009 baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mkundi iliyopo Mtwara.
Alipowasili Dar es Salaam hakuwa na shughuli maalumu ya kufanya kama walivyo vijana wengi ambao hutoka mikoani kuja Dar. Rajab naye alikuwa na ndoto ya kujitafutia maisha. Hivyo akajikita katika biashara ndogondogo akiamini kuwa akizifanya kwa umahiri na juhudi, zinaweza kumsaidia kupata fedha nyingi za kuanzisha biashara kubwa.
Akajikita katika biashara za kuuza chai na kahawa katika maeneo ya Kariakoo. Baadaye alifanya biashara ya kuuza nguo na vitu mbalimbali mitaani, yaani umachinga.
Lakini wakati wote huo ile nyota ya muziki ilikuwa ndani yake na ndiyo maana wakati akiendelea na biashara hizo alijitahidi na kurekodi nyimbo kadhaa, lakini kwa bahati mbaya hazikuwa na ubora uliokubaliwa na vituo vya radio wakati huo.
Harakati hasa za muziki alizianza mwaka 2011. Baada ya hapo akawa anajifunza kiasi mambo muhimu yanayohitajika ili mtu aweze kutoboa kupitia muziki.
Lakini kwa kuwa alikuwa anaendelea pia na zile biashara nyingine, ikawa vigumu kwake kupata muda wa kutosha kujiimarisha katika muziki, kwani hadi wakati huo alikuwa haamini kama angeweza kuendesha maisha kupitia muziki peke yake. Lakini hilo halikumkatisha tamaa. Aliamua kumtafuta mtu wa kumsimamia, yaani meneja. Hiyo ilikuwa ni miaka miwili kabla hajakubaliwa kujiunga WCB.
“Nimekwisha kurekodi nyimbo nyingi ndani ya lebo ya Wasafi, nimeona nianze kwanza na Aiyola huu uwe mwanzo wangu, pia nimejifunza vitu vingi kutoka kwa lebo ya WCB, kutoka kwa msanii Diamond Platnumz,” alitamka Harmozize wakati alipofanya mahojiano na vyombo vya habari miezi kadhaa baada ya kujiunga na WCB.
 
Historia ya maisha

Kwa upande wa historia ya maisha yake binafsi inaonyesha kufanana na ya meneja wake Diamond, kwa kuona umuhimu wa kusaidia vijana wengine na ndiyo maana akafungua studio nyumbani kwake na kuweza kuwasaidia vijana wanaochipukia katika fani ya muziki ambao hawana uwezo wa kifedha kuajiri maproducer wakubwa kuwasaidia kutoa kazi zao.
Harmonize aliwahi kusema kuwa wakati anajiunga WCB alijihisi kutumiwa, kwa sababu katika mambo mengi yaliyoihusu WCB alikuwa akitangulizwa yeye kama chambo.
“Unajua mimi katika WCB nilikuwa kama chambo, kwa sababu hata lebo ilipoanzishwa mimi ndiye niliyekuwa msanii wa kwanza kusaini, nikafanya vizuri wengine wakafuatia,” anasema na kuongeza:
“Hata kwenye mauzo ya muziki kwenye mtandao nimetangulizwa mimi. Lakini ninamshukuru Mungu kazi zimepokewa vizuri. Uongozi ulikuwa na mtazamo chanya tofauti na nilivyowaza.”
Msanii huyo anasema baada ya kiongozi wa lebo hiyo, Diamond Platnumz, kutoa albamu, yeye alidhamiria kuuomba uongozi wake na yeye afanye hivyo. Alijenga dhamira hiyo baada ya kuulizwa na waandishi alipofika Marekani kuwa ameshatoa albamu ngapi na kukosa majibu.
“Nilipokuwa Texas nchini Marekani, mdada mmoja aliniambia kuwa mimi ni msanii kutoka Tanzania, akaniuliza mpaka sasa nina albamu ngapi? Nikashindwa kumjibu kwa sababu sikuwa na albamu. Hii ilikuwa ni aibu, nikabaini kwamba ukiwa na albamu kadhaa lazima watu wakuheshimu,” anaeleza Harmonize.
Hilo likawa ni jambo jingine lililompa chachu ya kuongeza bidii katika muziki, hadi leo anajikuta akiwa ameinuka kutoka kijana aliyekuwa akiuza chai Kariakoo hadi kupigiwa chapuo na Rais Magufuli kuwa anafaa kugombea ubunge.
 
—Tamati—

By Jamhuri