Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mbunge wa viti maalum Stella Ikupa ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kusaidia makundi ya watu wenye uhitaji wakiwemo walemavu ambao wamekuwa na mahitaji mengi.

Aidha ametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watu wenye ualibino mkoani hapa ikiwemo mafuta maalum ya kuwalinda na mionzi ya jua inayosababisha saratani ya ngozi.

Ikupa, amekabidhi msaada huo jijini hapa kwa Mkurugenzi wa Shirika linalijihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu la Foundation For Disabilities Hope, (FDH) Maiko Salali.

“Leo nimekuja hapa kukabidhi msaada huu kwa watu wenye ulemavu vitu hivi ni mafuta maalum kwa watu wenye ualibino, kofia pamoja na miwani ambavyo vitawasaidi kujilinda na mionzi ya jua na kuondokana na tatizo la saratani ya ngozi”amesema Ikupa

Amesema, vifaa hivyo kwa watu wenye ualibino ni muhimu sana katika kulinda afya zao hivyo wadau wanapaswa kujiwekea utaratibu wa kusaidia kundi hilo mara kwa mara.

“Hivi vitu kwa watu wenye ulemavu ni kama chakula kwao watu mara nyingi wamekuwa wakihoji kwanini msaada kila siku lakini sisi watu wenye ulemavu vifaa hivi ni kama chakula kwetu hivyo msaada kama huu ni wa muhimu kwetu”amesema Ikupa

Ikupa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Ikupa Trust Fund, ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwezesha makundi ya watu wenye ulemavu.

Amesema, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu nchini ikiwemo kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.

“Hivi karibuni bungeni kupitia swali langu serikali ilieleza kuwa ipo kwenye mchakato wa kuchambua takwimu za watu wenye ulemavu kupitia sensa ya watu na makazi iliyofanyika 2022 ili kupata idadi kamili itakayowezesha serikali kuhudumia kundi hilo kikamilifu”amesema

Naye, Mkurunzi wa FDH, Maiko Salali amesema wanamshukuru mbunge huyo kwa msaada wa vifaa hivyo ambao vitakwenda kuwasaidia watu wenye ualibino mkoani hapa.

“Tunamshukuru sana mweshimiwa Ikupa kwa msaada huu na kwa namna amabavyo amekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wenye ulemavu na tunaahidi vifaa hivi vitawafikia walengwa wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali mkoani hapa”amesema Salali